Bunge la Somalia lakutana kumchagua rais mpya, milipuko yasikika Mogadishu

Matangazo ya kampeni za wagombea urais yakiwa yametanda katika mtaa mmoja mjini Mogadishu, Somalia.

Milipuko ilisikika Jumapili nje ya uwanja wa ndege wa Mogadishu nchini Somalia ambako bunge lilikuwa linakutana kumchagua rais mpya wa taifa  hilo katika upigaji kura ambao ni muhimu sana.

Uchaguzi huo ni sharti kwa nchi ya Somalia kuhakikisha misaada ya kigeni inaendelea kutolewa katika taifa hilo maskini ambalo limekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa takriban miongo mitatu.

Nusu dazeni ya wakazi na mwandishi wa habari wa Reuters walisikia milio iliyokuwa kama ya mizinga. Wasomali wamezoea mara kwa mara kuona mashambulizi kwenye taasisi za taifa ambayo yanafanywa na waasi wa kiislamu.

"Nilihesabu milio mitatu mikubwa ya makombora ikitua katika mwelekeo wa uwanja wa ndege. Tulishtushwa sana kusikia milio ya makombora wakati Mogadishu iko katika amri ya kutotoka nje. Nani alikuwa akiyafyatua?” alisema mmoja wa wakazi, Halima Ibrahim.

Hakuna ripoti zozote kuhusu uharibifu wowote au vifo.

Chanzo kimoja ndani ya uwanja wa ndege ambao una ulinzi mkali sana, ambako upigaji kura unafanyika, kimeliambia shirika la habari la Reuters hakuna milipuko ambayo imesikika ndani ya eneo hilo, ingawaje kulikuwa na kelele za ghasia wakati wa kuhesabu duru ya kwanza ya kura za wabunge.

Katika wagombea takriban 35 wanaowania nafasi ya juu ya uongozi, ni pamoja na marais wa zamani Sharif Sheikh Ahmed na Hassan Sheikh Mohamud walikuwa ni wagombea wa mbele, kwa mujibu wa wachambuzi, ingawaje tawala zao zilishindwa kuondoa rushwa au mizozo.

Upigazji kura unaoungwa mkono na Umoja wa mataifa ulicheleweshwa kwa zaidi ya mwaka kutokana na mivutano ndani ya serikali lakini lazima ufanyike mwezi huu ili kuhakikisha kuwa program za dola milioni 400 kutoka shirika la Kimataifa la Fedha zinaendelea.

Unafanyika wakati Somalia imekumbwa na ukame mbaya sana kuwahi kutokea katika kipindi cha takriban miongo minne, na dhidi ya mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na waasi wa al Shabaab, mapigano ya ndani miongoni mwa majeshi ya usalama na uhasimu wa koo.

Ingawaje kuutekeleza utaratibu huo ulikuwa na mafanikio kiasi, wengi nchini humo yenye watu takriban milioni 15 wana mashaka ya maendeleo ya kweli. Wagombea wanaoongoza ni wale wa zamani ambao wamefanya machache katika kuwasaidia, na upigaji kura kama huo kiutamaduni unatawaliwa na rushwa, walilalamika.

Rais aliyepo mamlakani Mohammed Abdullah, maarufu kama “Farmaajo” kwa sababu ya kuipenda jibini ya Italia formaggio, anaangaliwa kuwa si rahisi kuchaguliwa tena baada ya kupoteza uungaji mkono mwezi uliopita wakati wa kura ya bunge.