Boti hiyo ilikuwa imebeba wafanyabiashara na bidhaa zao wakitoka eneo la Mugote huko jimbo la Kivu Kusini na kwenda Goma mji mkuu wa jimbo jirani la Kivu Kaskazini.
Afisa wa polisi wa eneo la Mugote alisema upepo mkali ulisababisha mashua hiyo kuzama umbali wa kilomita 20 baada ya kuanza safari.
Afisa mwingine wa eneo hilo, kutoka Kivu Kusini, alisema mashua hiyo ilikuwa imebeba takriban abiria 150, 80 kati yao waliweza kujiokoa.
Alisema miili ya wanawake watatu na watoto watatu imepatikana wakati zoezi la kuwatafuta waathrika likiendelea.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ina barabara chache zinazopitika, hivyo usafiri wa kwenye maziwa na mito ni muhimu kwa kuyafikia maeneo mengi . Hata hivyo, ajali za meli zimekuwa ni jambo la kawaida nchini humo.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP