Mbunge wa Mbozi Pascal Haonga (Chadema) akizungumza bungeni leo, aliiomba serikali itoe ufafanuzi juu ya sababu zilizopelekea kufukuzwa mkurugenzi wa UNDP na kupewa saa 24 kuondoka nchini.
Lakini Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge aliliambia bunge kuwa serikali ina mamlaka yote katika masuala ya kidiplomasia na hivyo bunge haliwezi kuhoji sababu za mkurugenzi huyo kufukuzwa.
Mkurugenzi huyo raia wa Gambia, aliyeletwa nchini na Umoja wa Mataifa (UN) Agosti 2015, aliondolewa wiki iliyopita ndani ya saa 24 kwa agizo la Serikali, huku akiwa chini ya ulinzi.
Chanzo cha kuaminika kimeliambia gazeti la Mtanzania kuwa sababu ya kuondolewa kwa mkurugenzi huyo ni pamoja na hatua yake ya kuingilia baadhi ya mambo katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka 2015 pamoja na ule wa marudio wa Machi 20, mwaka jana.
Hatua hiyo inaelezwa kutowafurahisha baadhi ya viongozi wa Serikali.
“Kuondolewa kwa mkurugenzi huyo kumechangiwa pia na alichoandika katika ripoti yake kwenye Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu utata wa uchaguzi huo ambao Maalim Seif Sharif Hamad, aliulalamikia na kudai yeye ndiye mshindi.
“Si hilo tu, pia inaelezwa kuwa yapo baadhi ya matukio ambayo anatajwa nayo moja kwa moja ikiwemo kuwasikiliza baadhi ya viongozi walioshiriki uchaguzi na kushindwa, ikiwemo kuwapa mbinu za namna ya kuwasililisha malalamiko yao kwa vyombo vya kimataifa.
“Je, hata kama ungekuwa wewe unaingiliwa mambo yako ya ndani na mtu ambaye si raia wa nchi yako, unaweza kuvumilia? Jibu jepesi hapana,” kilisema chanzo hicho.
Agosti 2016, Maalim Seif alifanya ziara kimataifa katika nchi za Marekani, Ulaya, Canada na Umoja wa Mataifa kulalamikia uvurugaji wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015.
Kutokana na malalamiko yake, taasisi ya kimataifa ya Umoja wa Wanaliberali – Liberal International (LI) imeliandikia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) kutaka vikwazo dhidi ya Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa iliyopatikana kwenye tovuti ya LI, taasisi hiyo imetaka baraza hilo lenye jukumu la kulinda misingi ya haki za binadamu kwenye mataifa yote wanachama wa UN, kuchukua hatua kali ili kukomesha ilichokiita uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu na ukandamizaji wa haki za kisiasa na kiraia visiwani Zanzibar.
Katika tamko walilolitoa na kufikishwa mbele ya mkutano wa 33 wa baraza hilo uliofanyika Septemba mosi mwaka huu, Liberal International imetaka jumuiya ya kimataifa kufikiria kuweka vikwazo vya kusafiri na kuzuia mali za watu wote walioshiriki kuidhinisha vitendo vya utesaji wanasiasa wa upinzani na wafuasi wao