Kesi hiyo imekuja muda mfupi baada ya mahakama ya kijeshi kutupilia mbali kesi ya kumiliki bunduki na risasi na kumwachia huru.
Wine alikamatwa upya na kushtakiwa katika mahakama ya kiraia kujibu mashtaka ya uhaini pamoja na wabunge wengine walio kamatwa pamoja naye.
Mbunge huyo ambaye pia ni mwanamuziki nchini kwa jina maarufu Bobi Wine anakabiliwa na mashtaka mapya ya kujaribu kumdhuru Rais Museveni kwa kupiga mawe gari lake.
Yunus Ndiwalana, wa mahakama ya Gulu, ameeleza kuwa mahakama aliyopelekwa Wine haina uwezo wa kusikiliza kesi ya uhaini.
Wakati huo huo, viongozi wa upinzani akiwemo Dkt Kiiza Besigye nao wamekamatwa muda mfupi baada ya Wine kufunguliwa mashtaka.
Hata hivyo kumekuwa na shinikizo kubwa kimataifa la kutaka Bobi Wine aachiwe huru.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa kisiasa nchini Uganda, wanasema kesi inayo mkabili Wine ni jitihada za kumnyamazisha, kwani amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali tangu achaguliwe kuwa mbunge 2017.
Vyanzo vya habari vimeripoti kuwa mawakili wa jeshi wameeleza mahakama kuwa mashtaka dhidi ya Wine yameondolewa na sasa amekabidhiwa kwa polisi ili akafikishwe mahakamani kujibu mashtaka ya uhaini pamoja na na wabunge wengine walio kamatwa pamoja naye .