Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema leo kusiwepo na kitu chochote ambacho kitaondoa umuhimu wa kufikia sitisho la mapigano huko Gaza, baada ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh kuuwawa mapema nchini Iran.
Blinken ambaye yuko katika ziara rasmi Singapore kama sehemu ya kutembelea mataifa sita ya Asia amesema hawezi kubashiri kutakuwa na matokeo gani kwa tukio lolote moja kuhusiana na sitisho hilo la mapigano. Blinken amesema alipoulizwa kuhusu kifo cha Haniyeh kinaweza kuleta mivutano huko mashariki ya kati.
Mara nyingi Haniyeh anakuwa Qatar, amekuwa mstari wa mbele katika diplomasia ya kimataifa wakati vita vilivyochochewa na uvamizi wa Hamas huko Israel Oktoba 7 vikipamba moto Gaza.
Mauaji hayo yanakuja wakati kampeni za Israel Gaza zikikaribia kufikia mwisho wa miezi 10 kukiwa hakuna ishara yoyote ya kumalizika vita ambavyo vimetishia mzozo zaidi wa kikanda.