Binti wa shujaa wa ‘Mauaji ya Halaiki’ Rwanda aomba baba yake aachiliwe huru

Paul Rusesabagina

Siku ya Jumatatu asubuhi, Carine Kanimba binti wa mwanaharakati wa Rwanda Paul Rusesabagina alifahamu kuna jambo haliko sawasawa.

Alikuwa anapigiwa simu na marafiki wakimuuliza maswali kwa kushtushwa kwao na kile walichokiona katika taarifa za habari.

Alifungua televisheni na kujua kwa nini wamesitushwa.

“Tulimuona (baba) akiwa katika mikono ya serikali ya Rwanda, amefungwa pingu. Hivyo ndivyo tulivyojua hilo.”

Mwanaharakati huyu mwenye umri wa miaka 66 aliyekuwa ameonyeshwa katika filamu ya Hotel Rwanda alikamatwa mjini Dubai na kupelekwa katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Paul Rusesabagina akiwa mbele ya waandishi wa habari katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi ya Rwanda Kigali, Rwanda, Agosti. 31, 2020.

Akiwa amefuatana na maafisa wa polisi katika mkutano na waandishi wa habari, alifunguliwa mashtaka ya kufadhili makundi ya waasi na makosa yanayohusiana na ugaidi kati ya mambo mengine.

Alionekana katika ofisi za Idara ya Upelelezi za Rwanda, RIB, taasisi ya taifa ya kusimamia sheria.

“Tayari kulikuwa na hati ya kimataifa ya kutaka akamatwe. Hivyo basi atatakiwa kujibu tuhuma za uhalifu wa hali ya juu, kuchoma moto, utekaji na vitendo alivyosaidia vya mauaji dhidi ya raia wasio na silaha wa Rwanda katika ardhi ya Rwanda, ikiwemo eneo la Nyabimata [Mkoa wa Kusini mwa Rwanda], wilaya ya Nyaruguru mwezi Juni 2018 na huko Nyungwe, wilaya ya Nyamagabe mwezi Disemba 2018,” kaimu msemaji wa RIB, Thierry Murangira amekiambia kipindi cha radio cha Daybreak Africa, Idhaa ya Kiingereza katika Sauti ya Amerika.

Serikali ya Rwanda inamtuhumu Rusesabagina kwa kufadhili makundi makuu mawili ya upinzani, Rwandan Movement For Democratic Change, ambalo Rusesabagina aliliasisi na PDR-Ihumure.

“Amekuwa akifadhili misimamo mikali … makundi hayo ambayo yanaendesha harakati zao katika mikoa mbalimbali nje ya nchi. Wapi alipokanusha hilo?” Murangira amehoji.

Murangira hakueleza jinsi Rusesabagina alivyokamatwa, akisema “hatutaeleza habari zaidi kuhusu wapi alipokamatiwa, lakini naweza kuwaambia, amekamatwa kwa ushirikiano wa kimataifa.”

Mamlaka huko Umoja wa Falme za Kiarabu baadae walikanusha kuhusika na kukamatwa kwa Rusesabagina na kusema aliondolewa “kwa ndege binafsi iliyokuwa inaelekea nchi iliyoko Afrika Mashariki, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dubai, United Arab Emirates.

Safari ya Rusesabagina Dubai haiishangazi familia yake. Ikiwa ni sehemu ya harakati zake, anasafiri maeneo mbalimbali na kuzungumza katika taasisi mbalimbali amesema binti yake, ambaye alimchukua kumlea baada ya kuwa yatima kufuatia mauaji ya halaiki. Lililokuwa wazi kwa familia yake ni kwamba hakuwa amepanga kwenda Kigali.

“Kwenda Rwanda ilikuwa sio katika mpango wake kabisa. Na ndio sababu tunaamini alitekwa na kuletwa Rwanda,” amesema binti yake.

Rusesabagina ni raia wa Ubelgiji ana hati ya ukaazi wa kudumu Marekani, yaani Green Card. Haikufahamika jinsi alivyosafirishwa kutoka Dubai hadi Kigali.

Mara ya mwisho Kanimba alipozungumza na VOA kutoka Washington, alisema aliongea na baba yake kabla ya kusafiri kwenda Dubai Agosti 27.

“Nilikuwa nafahamu alikuwa akutane na baadhi ya watu kufanya mikutano michache na baadae alitakiwa kurejea siku ya Jumanne. Tarehe mosi Septemba,” amesema binti huyo kupitia mawasiliano ya Skype.

Siku hiyo ilikuwa siku ya kuzaliwa ya mpwa wangu na mjukuu wake … na alituma … ujumbe mzuri kwa mjukuu wake, akimtakia furaha ya siku ya kuzaliwa kwake.”

Mwanaharakati huyo alikuwa anawasiliana kupitia mtandao wa WhatsApp. Familia ilipokuwa inajaribu kumfikia kujua kama amewasili salama, ujumbe ulikuwa hauonyeshi umemfikia, amesema binti huyo.
“Hatukupata alama ya uthibitisho kwamba ujumbe ulimfikia, ambao kawaida tunapokea unapofanya mawasiliano.”

Mtandao wa WhatsApp umekuwa ukidukuliwa ambapo wapinzani na waandishi wamekuwa wakifuatiliwa na kufikiwa, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari.

‘Sijawahi kuhisi niko salama’

Rais Paul Kagame wa Rwanda

Katika miaka ya hivi karibuni mwanaharakati huyu amekuwa mkosoaji wa Rais wa Rwanda Paul Kagame. Katika kitabu cha maisha yake mwaka 2006, Rusesabagina ameandika, “Rwanda hivi leo ni taifa linaloongozwa na kikundi kidogo cha wasomi Watutsi kwa manufaa ya kikundi hicho.”

Wanafamilia wamekuwa kwa muda mrefu wakiamini Rusesabagina alikuwa anafuatiliwa kwa karibu na majasusi wa Rwanda wakati anaposafiri.

Mwaka 2016 alikiambia kipindi cha VOA Afrika 54, “Naweza kuwaambia sijawahi kuhisi niko salama tangu mwaka 2000. Nilipoanzisha harakati nikitembea ulimwenguni kuzungumzia kile kinachoendelea Rwanda wakati watu wengine wote walikuwa wamenyamazishwa.

Kwa hiyo, nilikuwa mtu pekee … nikifuatilia katika ofisi mbalimbali, nikiifikia jumuiya ya kimataifa kuwaeleza kile kinachoendelea nchini Rwanda.”

Wapinzani mbalimbali wa Rwanda, viongozi wa upinzani na maafisa wa zamani wa ngazi ya juu wameuawa ndani ya nchi na ughaibuni.

Katika ripoti yao ya mwaka 2019, taasisi ya kufuatilia haki za binadamu Human Rights Watch ilifanya uchunguzi huru juu ya mauaji hayo na kuwaomba wadau wa kimataifa kuweka shinikizo kwa serikali ya Kagame kuheshimu haki za binadamu.

“Katika ngazi ya kimataifa, Rwanda inaonekana ni mfano wa nchi yenye kufuata sheria na usalama, lakini tunashuhudia wimbi la vitendo vya uvunjaji sheria na wapinzani kushambuliwa bila ya Rwanda kuadhibiwa.

“Tofauti hiyo inastusha,” amesema.

‘Tusaidieni kumrejesha baba nyumbani’

Hivi sasa Kanimba anahofia usalama wa baba yake.

Ukweli wangu, ninahofu kubwa kwa usalama maisha yake. Yeye bado ni mgonjwa na alipambana na maradhi hayo ya saratani miaka michache iliyopita.

Ana tatizo la shinikizo la damu na anahitaji matibabu, chakula ambacho anatakiwa ale kabla ya kutumia dawa.

Binti yake anaomba msaada wa serikali ya Marekani na mataifa mengine duniani kusaidia baba yake kurejea nyumbani.

“Hatujui yuko katika hali gani hivi sasa,” amesema binti yake.

“Kwa hiyo tunaomba na kuisihi jumuiya ya kimataifa kutusaidia kumuona na kumsaidia arejee nyumbani.”