Kuachiwa Bilionea Dewji : Tayari ameungana na familia yake

Mohammed Dewji

Bilionea Mohammed Dewji amerejea nyumbani kwake mjini Dar es Salaam, Tanzania, baada ya kutekwa. Dewji alikuwa anashikiliwa na watu wasio julikana.

Taarifa zilizotolewa na Global Publishers Tanzania alfajiri Jumamosi, Oktoba 20, 2018, ni kuwa mfanyabiashara huyo ameachiwa na kurejea nyumbani kwake kuungana na familia yake akiwa salama.

Kwa mujibu wa mtandao wa Makampuni ya Mohamed Enterprises ya MeTL Group, Mo amerejea nyumba ikiwa ni siku ya tisa baada ya kutekwa na watu wasiojulikana Alhamis Oktoba 11 katika Hoteli ya Colessium iliyopo Masaki jijini Dar es salaam.

Akitoa taarifa hizo kuptia mtandao wa Twitter unaomilikiwa na Kampuni yake ya Mohamed Enterprises Ltd, Mo ameandika: “Namshukuru Mwenyezi Mungu nimerudi salama nyumbani. Nawashukuru Watanzania wenzangu na watu wote kote duniani kwa dua na sala zao. Nashukuru mamlaka zote, ikiwemo Jeshi la Polisi, zilizofanya kazi ya kuhakikisha narudi salama.” — Mohammed Dewji na , taarifa ambayo aliipost Saa 9:15 alfajiri, saa za Tanzania.

Aidha, Waziri wa Mazingira, Januari Makamba, nae kupitia mtandao wake wa Twitter, amethibitisha kupatikana kwa Mo na kusema kuwa mfanyabiashara huyo alitupwa maeneo ya Gymkhana huku akiwa na alama za kufungwa kamba mikononi.

“Nimemuona na kuongea kwa kirefu na Mohammed Dewji. Ni mzima wa afya isipokuwa ana alama za kufungwa kamba mikononi na miguuni. Mnamo saa nane usiku, watekaji waliamua kumtupa kwenye maeneo ya viwanja vya Gymkana. Naamini Polisi watatoa taarifa za ziada kuhusu kilichojiri.,” ameandika Makamba.