Rais wa Marekani Joe Biden atakutana Ijumaa na Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani na kiongozi mkuu wa amani Abdullah Abdullah katika Ikulu ya White House.
Mkutano huo wa kwanza wa ana kwa ana kati ya Biden na maafisa wa Afghanistan unakuja kabla ya kuondolewa kwa vikosi vilivyobaki vya Marekani na NATO kutoka Afghanistan ifikapo Septemba 11, kulingana na maamuzi ya Biden ya kufunga kile alichoelezea kama vita vya visivyokwisha.
Msemaji wa Ikulu Jen Psaki alisema mapema wiki hii kwamba Biden anatarajia kuwakaribisha viongozi wa Afghanistan na atawahakikishia msaada wa kidiplomasia, kiuchumi na misaada ya kibinadamu kwa nchi hiyo iliyokumbwa na machafuko wakati zoezi la kuwaondoa wanajeshi likiendelea.
Ghani na Abdullah walifika Alhamisi huko Washington na kukutana na viongozi wa baraza la Seneti Chuck Schumer na Mitch McConnell na wabunge wengine.