Kwa muda sasa balozi Godec amekuwa akisisitiza kuwa ni muhimu kuwepo mazungumzo yaliyo na uwezo wa kuwaleta wananchi wa Kenya pamoja.
Godec amekuwa kwenye harakati za kufanya mazungumzo na wahusika wakuu katika mgogoro huu, Jumatatu akikutana na wawakilishi wa Upinzani katika bunge baada ya kukutana na wabunge wa chama tawala cha Jubilee.
Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili ameripoti kuwa bado wengi wanajiuliza iwapo upo uwezekano wa Rais Kenyatta kumteua Odinga na vinara wenzake katika serikali yake.
Rais Kenyatta wiki iliyopita aliwateua mawaziri akiwemo Fred Matiang’i Waziri wa Usalama na kaimu Waziri wa Elimu, Joe Mucheru, Waziri wa Habari na Mawasiliano,Henry Rotich, Fedha ,Najib Balala, Waziri wa Utalii,Charles Keter, Kawi, na Waziri wa Uchukuzi James Macharia. Wengine aliowateua ni aliyekuwa mkurugenzi wa mashtaka ya Umma Keriako Tobiko, aliyekuwa gavana wa Marsabit Ukur Yattani pamoja na aliyekuwa Seneta wa Turkana John Munyes.
Baada ya kuteuliwa maafisa hao kuwa mawaziri, ripoti zimeibuka kuwa huenda Rais Kenyatta atafanya mazungumzo na upinzani kabla ya kuendelea na uteuzi wa mawaziri kadhaa.
Rais Kenyatta alionekana kusisitiza umuhimu wa utendaji wa maafisa wakuu anaotaka wafanikishe ndoto yake ya nguzo nne kuu katika awamu ya pili ya utawala wake.
Nguzo hizi zikiwa ni kupatikana kwa chakula cha kutosha kwa Wakenya, ujenzi wa nyumba bora na nafuu, upatikanaji rahisi wa huduma bora za kiafya na kuwepo kwa viwanda ili kuwapa wakenya kazi.
Harman Manyora, Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Nairobi na Mchanganuzi wa Siasa za Kenya anaeleza kuwa huenda Rais Kenyatta analegeza msimamo na kutaka kufanya mazungumzo na Odinga kufanikisha ajenda yake ya maendeleo.
Aidha, Manyora anasisitiza kuwa hatua ya Rais Kenyatta kutangaza maafisa sita pekee wa kuchukua nyadhifa za uwaziri katika serikali yake na kuwaacha wengine nje huenda ikawa ni sababu ya mvurutano kati yake na Naibu wake William Ruto.