Katika taarifa kwa vyombo vya habari, umoja huo ulimesema makubaliano hayo ni matokeo ya ziara ya mwezi Juni nchini Russia ya Mwenyekiti wa tume ya AU na rais wa Senegal Macky Sall, ambaye alisisitiza kwa Rais Vladimir Putin dharura ya kupelekwa nafaka kutoka Ukraine na Russia katika masoko ya dunia.
Mashamba ya Ukraine ni chanzo kikuu cha nafaka kwa soko la dunia, hasa katika Mashariki ya Kati na Afrika, ambapo, kwa sasa usambazaji wa chakula ni mdogo sana. Bei ya nafaka katika bara maskini zaidi duniani imepanda kwa sababu ya kudorora kwa mauzo ya nje, na hivyo kuongeza athari za migogoro na mabadiliko ya hali ya hewa na kuzua hofu ya machafuko ya kiraia.
"Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat anakaribisha kutiwa saini kwa makubaliano na Russia na Ukraine," ilisema taarifa hiyo, ikimsifu kiongozi wa Senegal na mwenyekiti wa AU Macky Sall "kwa kutoa wito wa hitaji la dharura la kuanza tena nafaka kutoka Ukraine."
Umoja wa Afrika pia umetoa wito wa kusitisha mara moja mapigano nchini Ukraine na kuanzishwa kwa mazungumzo mapya ya kisiasa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa kwa maslahi ya amani na utulivu duniani.
Haya yanajiri wakati bara hilo likiendelea kushuhudia uhaba mkubwa wa chakula.
Sall alimshukuru Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambaye alisimamia hafla ya utiaji saini mjini Istanbul siku ya Ijumaa, pamoja na marais Putin na Volodymyr Zelensky wa Ukraine.