Athari za risasi zapelekea Tundu Lissu kufanyiwa upasuaji wa 21

Tundu Lissu akiwa na ndugu na marafiki waliokwenda kumtembelea Hospitali ya Aga Khan nchini Kenya, 2017.

MBUNGE wa Singida Mashariki (Chadema) nchini Tanzania, Tundu Lissu anatarajia kufanyiwa operesheni ya 21 Jumamosi ili kuweza kuwekewa chuma (metal frame) kwenye mguu wake wa kulia.

Taarifa aliyoituma Ijumaa asubuhi kwenye mitandao ya kijamii, inaeleza kuwa atafanyiwa operesheni kuwekewa chuma hicho ili kiweze kushikilia vyema mguu wake ambao alifanyiwa upasuaji mwingine wa saa saba mwezi uliopita.

Alisema ingawa kwa sasa anaendelea vyema baada ya upasuaji kufanyika mwezi Juni, chuma kilipaswa kuwekwa wakati huo lakini ilishindikana baada ya kupoteza damu nyingi.

“Operesheni ya mwezi uliopita imepona, angalau kwenye muscles. Mfupa bado una kazi kubwa kidogo na utachukua muda kupona.

Itakumbukwa Lissu alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, mwaka 2017 nyumbani kwake wakati akiwa anahudhuria shughuli za bunge jijini Dodoma.

Alisema kazi ya kuweka chuma ni sehemu ya kukamilisha tiba ya mguu huo hivyo madaktari wanahitaji kuunga mfupa huo kwenye ‘metal frame’ itakayoushikilia ambayo atakaa nayo kati ya miezi sita hadi nane.

“Madaktari wangu wameniambia kwamba hiyo metal frame itakaa mguuni kati ya miezi sita hadi nane. Hata hivyo, haina maana kwamba nitakaa hospitalini kwa muda wote huo,”.

Lissu alisema baada ya upasuaji huo ataweza kuweka uzito wa mwili kwenye mguu na hatimaye atatembea bila magongo.

Alisema haina maana kuwa hataweza kufanya kazi yoyote kwa kipindi hicho bali atashauriana na madaktari, ndugu, familia, jamaa zangu na viongozi wenzake ili kuona mambo anayoweza kuyafanya wakati akiendelea na safari ya kupona.

Alisema mguu huo uliumizwa zaidi kwa risasi kwani ulivunjwa sehemu mbili na mfupa wa juu ya goti uliharibiwa hivyo kazi ya kuurekebisha ni ngumu.

Lissu aliwashukuru madaktari wakiwemo wale wa Nairobi na wa Ubelgiji kuwawalifanya kazi kubwa kuhakikisha wanautibu vyema mguu hadi kuweza kusimama, kutembea hata kama ni kwa kuchechemea kwa magongo.

“Safari bado ni ndefu, lakini sasa mwisho wake unaonekana more clearly (usahihi). Tulikotoka ni mbali na ni giza zaidi. Tunakoelekea ni karibu na kuna nuru kubwa zaidi,” alisema Lissu.

Lissu anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven nchini Ubelgiji ambako yuko huko tangu mwanzoni mwa Januari mwaka huu akitokea Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako alitibiwa kwa takribani miezi mine.

Mke wa Lissu, Alicia alinukuliwa na gazeti moja la kila siku nchini akisema kuwa mwanzoni mwa mwezi uliopita, mumewe huyo alifanyiwa upasuaji wa 20 ambao ulidumu kwa saa nane.