Chama cha African National Congress (ANC) kimepoteza wingi wake wa wabunge katika matokeo ya kihistoria ya uchaguzi Jumamosi ambayo yanaiweka Afrika Kusini kwenye mkondo mpya wa kisiasa kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa mfumo wa utawala wa kibaguzi wa wazungu walio wachache miaka 30 iliyopita.
Huku zaidi ya asilimia 99 ya kura zikiwa zimehesabiwa, ANC iliyokuwa ikitawala imepata zaidi ya asilimia 40 ya kura katika uchaguzi wa Jumatano, ambazo ni chache sana kwa zile ilizopata tangu uchaguzi wa mwaka 1994 ambao ulimaliza ubaguzi wa rangi na kumuingiza madarakani Nelson Mandela.
Matokeo ya mwisho bado hayaja tangazwa rasmi na tume huru ya uchaguzi iliyosimamia zoezi hilo lakini ni wazi kwamba ANC hakiwezi kupata zaidi ya asilimia 50.