Amnesty International yasema Niger imekiuka mkataba wa kuwalinda wakimbizi

Ramani ya Niger

Zaidi ya raia wa Sudan 100 waliokamatwa Nchini Niger wako hatarini kukabiliwa na vitendo vya unyanyasaji, ikiwemo kuwekwa kizuizini na mateso venye nia ya kuwataka walipe fedha kabla ya kuachiwa.

Vyanzo vya habari nchini Niger vinasema raia hao wanakabiliwa na uvunjifu wa sheria ikiwemo kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria katika mazingira magumu na aina nyengine za mateso, mara nyingi vitendo hivyo hufanyika ili kuwashinikiza watoe fidia ya fedha.

Hali hii inawakabili raia hao baada ya kurejeshwa nchini Libya wiki iliyopita, shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limeeleza.

Kikundi hicho cha watu takriban 145- wakiwemo wanawake na watoto- kiliondoka Libya kwa sababu ya vitendo vya kinyama ambavyo walikabiliwa navyo wakiwa hapo, na walikuwa wakiishi katika kambi za wakimbizi katika mji wa Agadez nchini Niger ambako walikuwa na matumaini ya kupata hadhi ya ukimbizi.

Mei 2, 2018 serikali ya Niger iliwakamata, na kuwapakia katika malori na kuwarejesha kwenye mpaka wa Libya. Mamlaka nchini Niger zimethibitisha kuondolewa kwa watu hao, wakisema kuwa hilo limefanyika kwa sababu watu hao hawakuwa “wakimbizi lakini ni wanachama wa makundi ya waasi wenye silaha ” nchini Libya, na hivyo wanahatarisha usalama wa nchi hiyo.

“Kwa kuwarejesha watu hao kwa nguvu Libya, serikali ya Niger imevunja msingi wa kuwalinda wakimbizi,” amesema Gaetan Mootoo, mtafiti wa shirika la Amnesty International Afrika Magharibi.

“Kwa kifupi Libya sio nchi salama. Utafiti wetu unaonyesha jinsi wakimbizi na wahamiaji wanavyokabiliwa na mateso, kuwekwa kizuizini na kutakiwa kulipa fidia. Serikali ya Niger lazima iwaruhusu watu hawa kurejea nchini humo kwa mujibu wa majukumu ya serikali chini ya mkataba wa wakimbizi na washirikiane na shirika la kusimamia wakimbizi la Umoja wa Mataifa kuwatafutia sehemu mbadala wakimbizi hao iliyokuwa salama,” amesema mtafiti huyo.

Msemaji wa Amnesty International alizungumza na mmoja wa raia hao wa Sudan walioondolewa Agadez ambaye alifanikiwa kutoroka baada ya zoezi hilo la kamakamata kufanyika.

Amesema alikuwa na mawasiliano na baadhi ya raia hao wa Sudan kwa njia ya simu na wamethibitisha kuwa tayari wameshapelekwa Libya.