Kupitia taarifa, Lansing alisema kuwa bodi hiyo itaendelea kuwaunga mkono raia wa Burundi kwa kutoa matangazo ya kuaminika na yasiyopotosha.
Taarifa hiyo ilifuatia hatua ya serikali ya Burundi ya kusitisha matangazo ya Sauti ya Amerika kwa muda wa miezi sita nchini humo kuanzia jana Jumatatu.
Hatua hiyo ilijiri siku moja baada ya dunia kuadhimisha siku ya Uhuru wa uandishi wa habari, na siku kumi tu kabla ya kura ya maoni nchini Burundi ambayo huenda ikabadilisha ukomo wa mihula ya urais.
Waandishi wa VOA nchini Burundi walithibitisha kwamba sitisho hilo lilianza kutekelezwa kama serikali ilivyokuwa imesema.
"Ingawa VOA pia hutangaza katika mawimbi ya masafa mafupi, televisheni na kupitia mtandao katika nchi hiyo, hapana shaka kwamba matangazo ya redio kupitia masafa ya FM ndiyo maarufu zaidi nchini Burundi," alisema Lansing.
Aliongeza kuwa raia wa Burundi wamekuwa wakitegemea Sauti ya Amerika kwa matangazo yasiyoegemea upande wowote, wakati nchi hiyo ikikabiliwa na mzozo unaoendelea wa kisiasa na wa kibinadamu.
"Ni muhimu sana kuendelea na matangazo hayo sasa, kuliko wakati mwingine wowote," alisema afisa huyo mwandamizi.