Haya yanajiri baada ya akina mama wazazi wa waandamanaji kukusanyika nje ya wizara ya sheria Jumanne kuwasilisha orodha ya waliouawa katika msururu wa maandamano yaliyofanyika kati ya mwezi Juni na Agosti.
“Tunachotaka kwa serikali yetu ni haki,” alisema Caroline Mutisya, ambaye alimpoteza mwanawe Erikson Kyalo.
Alisema “Tunataka maafisa wote wa polisi waliowauwa watu wakamatwe.”
Makundi ya haki za binadamu yanasema zaidi ya watu 60 waliuawa wakati wa wiki kadhaa za maandamano, yaliyochochewa awali na mswada wa fedha uliopendekeza nyongeza ya ushuru, huku wengine wakitoweka wiki kadhaa baada ya maandamano.
Maandamano ya amani yaliyoongozwa na vijana dhidi ya pendekezo la nyongeza ya ushuru yalichochea upinzani mkubwa dhidi ya rais William Ruto na kile ambacho wengi wanaona kama matumizi mabaya ya fedha za umma na ufisadi.