Vikosi vya Kenya vyaua al-Shabab 52 Somalia

Askari wa vikosi vya jeshi la Kenya wanaolinda amani nchini Somalia

Kambi ya wapiganaji wa al-Shabab imeshambuliwa na wapiganaji wake 52 kuuawa na silaha zao zote kukamatwa.

Operesheni hiyo imefanywa na vikosi vya Ulinzi vya Jeshi la Kenya huko Somalia chini ya majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa (AMISOM).

Tamko la Wizara ya Ulinzi Kenya limesema kuwa vikosi hivyo vilishambulia kambi hiyo iliyoko kilomita 9 Kaskazini mwa kijiji cha Sarira karibu na mji wa Badhadhe eneo la chini upande wa mkoa wa Jubba katika majira ya asubuhi Ijumaa.

“Operesheni iliongozwa na habari za kipelelezi ilitekelezwa baada ya vyombo vya usalama kugundua uwepo wa kundi kubwa la magaidi wa al-Shabab katika eneo hilo,” imesema taarifa hiyo iliyokuwa imepostiwa katika akaunti yake ya twitter.

“Majeshi ya ardhini yakisaidiwa na mashambulizi ya makombora na mabomu yalitumika kusafisha kambi hizo baada ya hapo,” taarifa hiyo iliongezea.

Mkazi wa eneo ambaye hakuweza kutambuliwa kwa jina kwa sababu za usalama ameiambia VOA kuwa sehemu ambako shambulio hilo hasa lilitokea ni Sangabo, ni msitu wa pembe tatu kati ya maeneo ya Badhadhe, Kulbiyow na Raskamboni.

Amesema vikosi vya Kenya vilitumia helikopta kushambulia kwa mabomu eneo hilo mapema asubuhi na kusema kuwa mashambulizi ya anga katika eneo hilo yanaendelea.

Mkazi huyo amesema kuwa kambi ya al-Shabab iko karibu na Lagta Dishu ambayo ni kituo cha jeshi kinachotumika na majeshi ya Kenya yanayofanya operesheni zake nchini Somalia.

Mkazi huyo hakuweza kuthibisha idadi ya vifo vya wapiganaji wa al-Shabab iliotolewa na jeshi la Kenya.

“Inawezekana kuwa wapiganaji wa al-Shabab waliuawa lakini sijui idadi yao,” amesema.

Kenya imesema kuwa wapiganaji wengine walikimbia hali wakiwa wamejeruhiwa.

Tamko La jeshi hilo limesema kuwa vikosi vyake vilikamata silaha zikiwemo bunduki aina ya AK47, risasi na mabomu.

Badhadhe iko kilomita 200 kusini magharibi ya Kismayo na ni mmoja ya miji mkuu ambao uko chini ya kikundi cha wapiganaji wa al-Shabab.