Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, waziri wa sheria wa Congo amewatishia wanahabari na wale wanaoripoti kuhusu M23 kwa adhabu ya kifo, ingawa hakuna sheria inayovizuia rasmi vyombo vya habari kuripoti kuhusu makundi ya waasi.
Aljazeera yenye makao makuu Doha, Qatar kufikia sasa haijatoa maoni yoyote kuhusu hatua hiyo. Kulingana na msemaji wa serikali ya Congo Patrick Muyaya, serikali ilifuta vibali vya uandishi vya Al Jazeera nchini humo, akisema kuwa mtandao huo ulimhoji kiongozi wa “ kundi la kigaidi bila kupata idhini.
Jumatano Al Jazeera ilirusha mahojiano na Bertrand Bisimwa ambaye ni kiongozi wa M23 mashariki mwa Congo, ambapo aliilaumu serikali ya Congo kwa kukiuka makubaliano ya sitisho la mapigano la Agosti, na hivyo kudai kwamba kundi lake limelazimika kuendelea na mapigano.
M23 ndilo lenye nguvu zaidi kati ya zaidi ya makundi 100 ya uasi yaliyopo kwenye mpaka kati ya Congo na Rwanda ambapo zaidi ya watu milioni moja walitoroka makwao kutokana na mapigano mwaka uliopita. Eneo hilo lina utajiri mkubwa wa madini.