Safari hiyo imeanza baada ya kusitishwa kwa miezi 18 tangu vita vilipoanza kwenye eneo hilo.
Tangazo hilo limetolewa siku moja baada wajumbe wa ngazi ya juu wa serikali kufanya ziara ya kwanza mkoani humo tangu kutiwa saini kwa mkataba wa amani mwezi uliopita.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la ndege la Ethiopian Airlines, Mesfin Tasew amesema kwamba safari mpya za ndege zitaziunganisha tena familia, kurejesha biashara, pamoja na kuvutia watalii, kwa manufaa ya jimbo hilo.
Tayari misaada imeanza kumiminika tena katika mkoa wa Tigray tangu kutiwa saini kwa mkataba wa amani Novemba 2, na hivyo kupunguza uhaba mkubwa wa chakula uliokuwa unashuhudiwa, pamoja na fedha , mafuta na dawa.
Hata hivyo eneo hilo lenye takriban wakazi milioni 6 bado halina huduma za umeme, simu, internet na benki kwenye maeneo mengi.