Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov, amesema Rais wa Russia Vladimir Putin anatarajiwa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy wiki hii.
Lavrov amesema kwamba mazungumzo hayo yanayotarajiwa kufanyika Uturuki, yatakuwa na manufaa kwa nchi zote mbili.
"Putin amesema kwamba hajawahi kukataa kukutana na rais Zelensky. Kitu pekee anachokifikira kuwa muhimu ni kwamba mkutano kama huo ni lazima upangwe vizuri. Kwa sasa, hali ni kwamba kuna mgogoro mkubwa nchini Ukraine. Mgogoro huo umekuwepo kwa muda mrefu na matatizo yamekuwa yakiongezeka. Hiyo ndio sababu ni vyema wakutane na wabadilishane mawazo," amesema Lavrov.
Kremlin imesema kwamba mazungumzo ya amani kati ya Russia na Ukraine huenda yakafanyika kesho Jumanne nchini Uturuki, na kwamba ni muhimu kuwa yanafanyika ana kwa ana.
Uvamizi wa Russia nchini Ukraine umeingia siku ya 33.
Waokoaji wanaendelea kutafuta miili ya watu chini ya majengo yaliyoharibiwa kutokana na mashambulizi ya mabomu.
Japo wanajeshi wa Ukraine wametwaa kijiji cha Bashatanka kutoka kwa wanajeshi wa Russia, kijiji hicho kimeharibiwa vibaya kutokana na vita hivyo.
Suala kuu katika mazungumzo kati ya Zelenskyy na Putin, litakuwa uhuru wa Ukraine.
Umoja wa Mataifa unakadhiria karibu raia 1,100 wamekufa na zaidi ya watu milioni 4 kutorokea nchini jirani kutokana na mapigano hayo.
Habari hii inatokana na vyanzo mbalimbali vya habari.