Rais wa Marekani Joe Biden aliweka vikwazo vya ziada Alhamisi ambavyo alisema vitakuwa na gharama kubwa sana kwa uchumi wa Russia kufuatia uvamizi wa Rais wa Russia Vladmir Putin nchini Ukraine.
“Putin ndie mchokozi, Biden alitangaza akiwa White House. Putin alichagua vita hivi, na hivi sasa yeye na nchi yake watakumbana na matokeo”. Vikwazo vipya vinalenga mabenki ya Russia, wafanyabiashara tajiri wenye ushawishi wa kisiasa, na sekta za teknolojia ya juu.
Biden alisema kwamba baada ya muda vikwazo hivyo vitazuia mali za Russia na kudhoofisha ukuaji wake wa uchumi kwa miaka ijayo. Itakuwa pigo kubwa kwa matarajio yao ya muda mrefu. Kiongozi huyo wa Marekani alikiri madereva wa Marekani watakumbana na bei za juu za petrol kwa sababu ya kupanda kwa bei ya mafuta duniani kulikosababishwa na uvamizi wa Russia dhidi ya Ukraine.
Lakini Rais Biden alisema uchokozi huu hauwezi kuachwa bila kujibiwa. “Marekani inasimamia uhuru. Hivi ndivyo tulivyo”.