Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Novemba 25, 2024 Local time: 12:46

Viongozi wa Ulaya wasema hakuna ishara Russia inaondosha majeshi yake


Vokosi vya Russia vinaendelea na mazoezi ya kijeshi mpakani na Ukraine
Vokosi vya Russia vinaendelea na mazoezi ya kijeshi mpakani na Ukraine

Viongozi wa Ulaya wanasema hakuna ishara zozote kuonyesha Russia inaondosha wanajeshi wake kutoka mipaka ya Ukraine, huku Rais Joe Biden wa Marekani akionya kwamba iko tayari kujibu vikali.

Jana Moscow ilitangaza kwamba inaanza kuondoa sehemu ya wanajeshi na vifaa vyake vya kijeshi baada ya kukamilisha zoezi kubwa nchini Belarus na hii leo kutangaza kukamilisha mazoezi kwenye peninsula ya Crimea.

Katibu mkuu wa muungano wa NATO, Jens Stoltenberg, akizungumza kabla ya mkutano na mawaziri wa ulinzi amesema wako tayari kwa hali yoyote itakayojitokeza na Russia itakumbwa na hasara kubwa ikithubutu kuivamia Ukraine.

Katibu mkuu wa NATO anaeleza: "Tutaendelea kupeleka ujumbe uliyo wazi kabisa kwa Russia kwamba sisi tuko tayari kukaa chini kwa mazungumzo pamoja nao. Lakini wakati huo huo, tuko tayari kukabiliana na hali yoyote mbaya itakayotokea."

Jens Stoltenberg
Jens Stoltenberg

Wito kama huo ulitolewa pia hii leo na kamishna wa Umoja wa Ulaya Ursula Von Der Leyen alipokuwa analihutubia bunge la Umoja wa Ulaya leo Jumatano.

Der Leyen ameeleza haya: "Umoja wa Ulaya na washirika wetu upande wa pili wa Atlantiki tumeungana katika kukabiliana na mzozo huu na wito wetu kwa Russia ni bayana kabisa usichague vita. Njia ya ushirikiano kati ya Russia na sisi unaweza kufanyika. Lakini tubaki makini. Kwani licha ya habari za jana, NATO haijaona bado dalili za kupunguza kwa wanajeshi wa Russia."

Hapo jana wizara ya ulinzi ya Russia ilitangaza kwamba inaondoa baadhi ya wanajeshi wake na vifaa vya kijeshi kutoka Belarus baada ya kukamilisha zoezi la kijeshi. Na hii leo imetoa video nyingine ikionyesha kuondolewa kwa vifaa vyake kutoka peninsula iinayoikalia ya Crimea.

Akiwahutubia wamarekani kwa mara ya kwanza tangu kuzuka kwa mvutano huu Rais Joe Biden alisisitiza kwamba hakuna mabadiliko kwenye mpaka kati ya Russia na Ukraine na hawawezi kuthibitisha bado kwamba wanajeshi 150,000 wameanza kuondolewa.

Rais Biden anaeleza: Ikiwa Rashia itaendelea na mipango yake, tutaungana pamoja kupinga uvamizi wake, Marekani na washirika wake kote duniani wako tayari kuiwekea vikwazo vikali dhidi ya bidhaa zake zinazosafirishwa nje, pamoja na hatua nyinginezo, hatukufanya chochote ilipovamia mashariki mwa Ukraine 2014.

Rais Joe Biden
Rais Joe Biden

Rais Biden aliwaonya pia Wamarekani kwamba hatua kama hizo zitakuwa pia na gharama kubwa hapa nyumbani wakitarajia kushuhudia kuongezeka kwa bei za bidhaa pamoja na mafuta.

Msemaji wa Kremlin Dimitry Peskov amefurahia pendekezo la rais Biden la kutaka mazungumzo juu ya kupunguza mivutano.

Dimitry Peskov Msemaji wa Kremlin amesema: "Mnafahamu kwamba Rais Putin amesisistiza matarajio na utayari wetu wa kushiriki kwenye majadiliano kama hayo. Na kwa vile Rais wa Marekani ametangaza dhamira yake ya kuanza mazungumzo ya dhati ni jambo chanya.

Huko Ukraine kwenyewe wananchi wanasherekea siku ya Umoja kwa kukusanyika kwenye uwanja mkuu wa Kyiv na kufungua bendera ndefu ya nchi yao kuonyesha uzalendo wao na tayari kuilinda nchi yao. Rais Volodymyr Zelenskyy mapema wiki hii alitangaza Februari 16 ni siku ya umoja ikiwa siku ilidhaniwa Russia itaanza uvamizi wake.

XS
SM
MD
LG