Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 16:00

Marekani yasema Russia huenda ikaivamia Ukraine kabla ya Jumatano


Rais wa Russia Vladmir Putin (Kushoto) na Rais wa Marekani Joe Biden (Kulia).
Rais wa Russia Vladmir Putin (Kushoto) na Rais wa Marekani Joe Biden (Kulia).

Rais wa Marekani Joe Biden na Rais wa Russia Vladimir Putin wamepangiwa kufanya mazungumzo kwa njia ya simu Jumamosi wakati mvutano inaendelea kuongezeka huku kukiwa na wasiwasi kwamba Russia iko tayari kuivamia Ukraine.

Washington imepokea taarifa za kipelelezi kuwa uvamizi unaweza kutokea mapema Jumatano.

Ubalozi wa Marekani mjini Kyiv umeanza kuwaondoa wafanyakazi wake. Kwa kuongezea, Wizara ya Mambo ya Nje imetoa tahadhari ya kusafiri ikionya watu kutokwenda Ukraine “ kutokana na kuongezeka kwa vitisho vya hatua za kijeshi za Russia” na kuwashauri “ wale wote walioko Ukraine kuondoka mara moja.”

Wanadiplomasia wachache wa Marekani walitarajiwa kuhamishiwa eneo la mbali la magharibi mwa Ukraine, karibu na Poland, mshirika wa NATO, kitu ambacho itakiwezesha Marekani kuendelea “kufanya shughuli za diplomasia” huko Ukraine.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Russia Maria Zakharova alisema Jumamosi kwamba Moscow imeamua “kuongeza” idadi ya wafanyakazi wake kidiplomasia nchini Ukraine, akielezea hofu ya “uwezekano wa uchokozi kutoka kwa utawala wa Kyiv.”

Zakharovahakutoa maelezo zaidi kuhusu hatua hiyo lakini amesema ubalozi huo na balozi zake ndogo nchini Ukraine ziliendelea kutekeleza majukumu yake muhimu.

Pia siku ya Jumamosi, Uingereza imewaambia raia wake kuondoka Ukraine, na Ujerumani na Uholanzi imewaambia raia wake kuondoka haraka iwezekanavyo.

Kabla ya viongozi hao wawili kufanya mazungumzo Jumamosi, Putin atazungumza na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye Putin alikutana naye mapema wiki hii.

Mapema Jumamosi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken alisema ataongea na waziri mwenzake wa Russia, Sergey Lavrov, Jumamosi kuhusu kile ambacho kinaonekana kuwa uvamizi usiokuwa na shaka wa Russia kwa Ukraine.

Blinken, akiongea katika mkutano wa waandishi wa habari huko Fiji, alisema kama Putin “ataamua kuchukua hatua za kijeshi [dhidi ya Ukraine] tutaiwekea vikwazo vikali vya kiuchumi kwa kushirikiana na washirika na wadau wetu kote ulimwenguni, tutaimarisha uwezo wa Ukraine kujihami, tutaongeza nguvu kwa washirika wetu upande wa mashariki. Nitasisitiza umoja huu na matokeo nitakapoongea na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Lavrov baadae usiku.”

Mshauri wa usalama wa taifa wa White House Jake Sullivan amesema Ijumaa kwamba uvamizi wa Russia nchini Ukraine unaweza kuanza “wakati wa michezo ya Olimpiki” au pale Putin atakapo amua kuamuru hilo kufanyika.

Wachambuzi wengi wamesema kuwa Russia siyo rahisi kufanya uvamizi wowote kabla ya michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi kumalizika Februari 20.

Russia hivi sasa ina wanajeshi wa kutosha kwenye mpaka wa Ukraine ili kutekeleza operesheni kubwa ya kijeshi, Sullivan amesema, Russia inaweza kuvamia “eneo muhimu” la Ukraine, ikiwemo mji mkuu, Kyiv, katika shambulizi hilo.

Siku ya Ijumaa, Biden alishiriki katika mazungumzo salama kwa njia ya video na viongozi wa dunia kujadili suala la Ukraine.

“Viongozi hao walikubaliana juu ya umuhimu wa kuratibu juhudi zao kuzuia uchokozi zaidi wa Russia dhidi ya Ukraine, ikiwemo utayari wao kwa kuweka vikwazo vikubwa na kusababisha gharama kubwa sana ya uchumi kwa Russia iwapo itachagua kuzidisha hatua za kijeshi,” kwa mujibu wa taarifa ya White House.

Mbali ya Biden katika mazungumzo hayo walikuwepo viongozi wa Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Poland, Romania, Uingereza, NATO, Umoja wa Ulaya na Baraza la Ulaya.

XS
SM
MD
LG