Maafisa wa usalama wa Sudan wamewaua kwa risasi waandamanaji wawili walipokuwa wanajaribu kuwatawanya maelfu ya waadamanaji, kwa kutumia gesi ya kutoa machozi kwenye mji mkuu wa Khartoum pamoja na mji pacha wa Omdurman siku ya Jumatatu.
Kamati ya Madaktari wa Sudan inasema mwandamanaji huyo aliuawa kwa kupigwa risasi kifuani na kufikisha idadi ya waliouawa na polisi wakati wa maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana kufikia 80. Maandamano hayo yanasemekana yamefanyika pia kwenye maeneo mengine ya nchi ikiwemo Darfur magharibi.
Mjini Khartoum waandamanji walibeba bendera ya Sudan pamoja na mapulizo mekundu ikiambatana na siku ya Valentine, na wengine wakibeba picha za watu walouliwa tangu kuanza maandamano mwaka 2021.
Waandamanaji wamekuwa pia wakiimba nyimbo za kuitaka serikali kuachalia huru watu waliokamatwa baada ya mapinduzi ya kijeshi mwezi Oktoba mwaka jana. Maafisa wa usalama walilazimika kutumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya waandamaji waliokuwa wamekusanyika karibu na makao ya rais mjini Khartoum.
Maandamano ya Jumatatu yamechochewa zaidi na kukamatwa Jumapili kwa Mohamed al Fekki ambaye alikuwa moja wa wajumbe kwenye baraza la utawala lililoongoza serikali ya kiraia kwa ushirikiano na jeshi baada ya kiongozi wa muda mrefu Omar al Bashir kuondolewa madarakani mwaka wa 2019.
Mbali na kukamatwa al Fekki kuna wengine waliokamatwa wiki iliyopita ikiwa ni pamoja na aliyekuwa waziri Khalid Omar Youssef pamoja na Wagdi Saleh ambaye ni msemaji wa muungano wa mashirika ya kiraia wa Forces for Freedom and Change, FFC.
Chama cha wafanyakazi wenye Uledi cha Sudan SPA kwamba "idadi ya wanaharakati walokamatwa bila ya mashtaka ya uhalifu imepindukia 100 hivi sasa."
Maandamano hayo yamefanyika siku moja baada ya mkuu wa Baraza la Utawala la Sudana Jenerali Abdel Fattah Burhan kukutana na mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat mjini Khratoum ili kuzungumzia juu ya hali ya kisiasa nchini humo.
Faki halikadhalika alikutana Jumatatu na viongozi wa vyama vya upinzani wakati wa ziara ya siku mbilli nchini humo.