Rais Barack Obama anafanya ziara yake ya kwanza baadae mwezi huu nchini Ethiopia na makao makuu ya Umoja wa Afrika. Ni mara ya kwanza kwa Rais wa Marekani aliyeko madarakani kutembelea taasisi hiyo ya afrika ambayo inazidi kupaza sauti kuzungumzia masuala ya Afrika.
Ziara ya tatu ya Rais Barack Obama barani Afrika itamchukua hadi mahala ambako hakuna rais yeyote wa Marekani aliye mamlakani ameshakwenda hapo kabla, ndani ya ofisi za Umoja wa Afrika.
Bwana Obama atasafiri kuelekea Addis Ababa, makao makuu ya AU kama sehemu ya safari yake ambayo itampeleka hadi Kenya.
Atakutana na viongozi wa mataifa yote mawili pamoja na viongozi wa Umoja wa Afrika.
Wachambuzi wanasema kwamba akiwa AU, bwana Obama ataendelea na majadiliano ya serikali yake juu ya mapambano ya ugaidi na kuboresha maendeleo na demokrasia.
David Zounmenou wa taasisi inayohusika na usalama alisema “mapambano dhidi ya ugaidi ambayo yamekuwa muhimu sana na suala la kubadilishana utawala kwa njia ya kidemokrasia barani Afrika. Kwa hakika hii ni fursa muhimu ya kuelezea tena msimamo wa Marekani juu ya masuala hayo makuu mawili muhimu na kupeleka ujumbe mzito kwa viongozi wa Afrika ambao wanataka kuendelea kuwepo madarakani”.
Marekani na Umoja wa Afrika si kwamba wanakubaliana wakati wote. Marekani inapinga vikali suala la AU kukataa kumkamata Rais wa Sudan anayetafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC wakati alipohudhuria mkutano wa hivi karibuni wa Umoja wa Afrika mjini Johannesburg.
Marekani pia inapinga majaribio ya baadhi ya viongozi wa Afrika kujiongezea mihula yao ya madarakani, kwa kubadili au kukiuka katiba zao kama inavyoonekana hivi sasa huko Burundi.
Lakini maafisa wa Marekani wanasema heshima kubwa kwa Umoja wa Afrika.
Waziri mdogo wa mambo ya nje wa Marekani kwa masuala ya Afrika, Linda Thomas-Greenfield alisema “ni taasisi yenye mafanikio na bado inakazi kubwa ya kufanya. Inaheshimika barani humo na ninafikiri wakati tunapoangalia mbele agenda za AU kwa mwaka 2063, tutaona AU inakuwa na nguvu zaidi barani humo”.
Wachambuzi wanasema Marekani inaihitaji AU kama ambavyo AU inavyoihitaji Marekani, mfadhili mkubwa wa taasisi hiyo.
Lakini baadhi pia wanaeleza kwamba Afrika ina masuala mengine mengi.
Mchambuzi kwa masuala ya Afrika Liesl Louw-Vaudran alisema “Marekani bila shaka inaihitaji AU kama inataka kufanya kazi na bara la Afrika, kufikia makubaliano , na kuwa mpinzani wa China”.
Kwa sababu hiyo na nyingine, hii itakuwa ziara ya kihistoria kwa bwana Obama na moja ambayo inaonekana ni kusaidia kutengeneza urithi wake, kama rais wa kwanza wa Marekani mwenye ushirikiano wenye nguvu na bara la Afrika.