Watu 42, akiwemo mtangazaji maarufu wa radio na televeshini na vijana watatu viongozi wa maandamano hayo, walifikishwa kwa haraka mahakamani na kuwekwa rumande chini ya ulinzi wa polisi kwa mashtaka yakiwemo yale “ya kuwa kero”, walisema.
Rais Yoweri Museveni, ambaye ameliongoza kimabavu taifa hilo la Afrika Mashariki kwa takriban miongo minne, alikuwa ameonya mwishoni mwa Juma kwamba waandamanaji “wanacheza na moto”.
Polisi wa kukabiliana na ghasia walionekana kwa wingi mjini kote Kampala, wakiweka vizuizi vya barabarani hasa karibu na eneo la biashara, huku maafisa wa usalama wakifunga barabara inayoelekea bungeni.
Msemaji wa polisi Kituuma Rusoke alisema mamlaka hazitoruhusu maandamano yoyote ambayo yanatishia “amani na usalama wa Uganda”.
Maandamano ya kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya ufisadi yaliandaliwa na vijana wa Uganda kupitia mitandao ya kijamii, huku kukiwa na mabango yenye rangi mbalimbali yakiwataka watu kuandamana hadi bungeni, kwa kuiga mfano wa maandamano ya kupinga serikali katika nchi jirani ya Kenya yanayoongozwa na vijana wanaojulikana kama Gen-Z.
Rushwa ni tatizo kubwa nchini Uganda, huku kukiwa na kashfa kadhaa zinazohusisha viongozi wa ngazi ya juu na maafisa wa umma, na nchi hiyo imeorodheshwa nafasi ya chini ya 141 kati ya nchi 180 kwenye ripoti ya shirika la Transparency International linalopiga vita ufisadi.
Forum