Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 17:45

Watu 22 Tanzania 'wafa maji' Ziwa Tanganyika


Ziwa Tanganyika nchini Tanzania
Ziwa Tanganyika nchini Tanzania

Watu 22 wanahofiwa kufa maji Ziwa Tanganyika, nchini Tanzania katika ajali ya boti iliyotokea Jumamosi alfajiri.

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) Mkoa wa Kigoma, imesema ajali hiyo ilitokea katika kitongoji cha Lubengela kijijini Msihezi, Kata ya Sunuka wilayani Uvinza.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimeongeza kuwa miili ya watu wanne iliopolewa na imetambuliwa na ndugu zao, huku watu wengine 115 wameokolewa wakiwa hai baada ya boti kugonga mashuwa.

Mashuwa hiyo ijulikanayo kama Mv Pasaka iligongwa ubavuni na boti ya Atakalo Mola na kupasuka, hivyo kuzama ziwani.

Sumatra imesema mashua hiyo ilikuwa imebeba abiria 137 waliokuwa wanakwenda kwenye mkutano wa injili katika Kijiji cha Sunuka.

Kwa mujibu wa Sumatra boti ilikuwa ikitokea Kigoma kwenda Kalya ikiwa imebeba abiria 65.

Sheria za usafiri wa majini haziruhusu mitumbwi inayobeba abiria kufanya safari usiku.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Sweetbert Njewike akizungumzia ajali hiyo amesema wanaendelea kuwatafuta watu ambao hawajaonekana waliokuwa wakisafiri na vyombo hivyo.

Amesema shughuli za uokoaji zinafanywa kwa pamoja na vikosi vya Polisi, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mwanamvua Mrindoko amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kulikuwa na dosari zilizosababisha ajali hiyo.

Amezitaja dosari hizo kuwa ni ukosefu wa vifaa vya uokoaji, vifaa vya kuzima moto na boti kufanya safari usiku.

XS
SM
MD
LG