Ajali ya basi kwenye barabara kuu nchini Misri iliua watu 12 na kujeruhi wengine 33 Jumatatu, wizara ya afya ya nchi hiyo ilisema katika taarifa.
Basi hilo lilikuwa limebeba wanafunzi waliokuwa wakirudi nyumbani kutoka Chuo Kikuu cha Galala katika jimbo la Suez mashariki mwa Misri, wakati lilipopinduka kwenye barabara kuu, gazeti linalomilikiwa na serikali Akhbar al-Youm liliripoti.
Hapakuwa gari lingine lililohusika katika ajali hiyo, na uchunguzi umeanzishwa kubaini kasi ya basi hilo na mazingira ya ajali hiyo, gazeti hilo lilisema.
Wizara ya afya ilisema waliojeruhiwa walipelekwa kwenye hospitali iliyo karibu, 19 kati yao waliondoka hospitali Jumatatu jioni.
Ajali za barabarani ni jambo la kawaida nchini Misri, ambako madereva mara nyingi hupuuza sheria za usafiri wa barabarani na barabara nyingi ziko katika hali mbaya.
Barabara ya Galala ambako ajali hiyo ilitokea, hata hivyo, ni moja ya maelfu ya kilomita ya barabara kuu na njia za juu zilizojengwa katika mwongo mmoja uliopita, kama sehemu ya kipaumbele cha serikali katika miradi ya miundombinu.
Takwimu rasmi zinasema zaidi ya watu 5,600 waliuawa katika ajali za barabarani mwaka 2023 katika taifa hilo lenye idadi ya kubwa zaidi ya watu katika mataifa ya Kiarabu.
Forum