Haya yamejiri wiki mbili tu baada ya wanasiasa wengine wawili kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa tuhuma za kutoa matamshi ya chuki, kufuatia mchakato wa uchaguzi mkuu uliondaliwa nchini humo Agosti 8, 2017.
Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa Paul Ongili, almaarufu Babu Owino, ambaye ni mbunge wa Embakasi Mashariki jijini Nairobi, amekuwa mwanasiasa wa pili kukamatwa na maafisa wa polisi chini ya saa 24 baada ya aliyekuwa mbunge wa Nakuru mjini David Manyara kukamatwa kwa tuhuma za kutoa matamshi yenye chuki.
Babu Owino aliripotiwa kutoa matamshi yanayoonekana kumdhalilisha Rais Kenyatta katika mkutano wa hadhara jijini Nairobi.
David Manyara ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Jubilee katika Kaunti ya Nakuru, anatuhumiwa kutoa matamshi ya chuki dhidi ya Jamii moja humu nchini yenye ushawishi mkubwa wa kisiasa.
Kukamatwa kwa wanasiasa hawa kunajiri tu takriban wiki mbili baada ya kukamatwa kwa Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama kwa tuhuma za kutoa matamshi ya uchochezi.
Na japo Babu Owino hadi tukienda hewani alikuwa anazuiliwa katika makao makuu ya taasisi ya uchunguzi nchini, David Manyara aliachiliwa kwa dhamana ya laki moja.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya.