Wakati Ufaransa ikifunga goli la pili, kelele zilizoziba masikio za uungwaji mkono kupindukia wa Morocco ndani ya uwanja wa mpira wa Al- Bayt wa Qatar zilizimika – kimya kilichopita siyo tu Rabat na Casablanca, lakini huko Beirut, Cairo na Dakar.
Mwanamke aliyekuwa amevalia nguo ya kijani, akiwa amekaa katika mistari ya wafuasi waliokuwa wakipiga miluzi, ngoma na wakisherehekea kupitia mechi hiyo, aliketi kimya, mikono yake ikishikilia mbele ya midomo yake kutizama kipute hicho cha dakika za mwisho.
Katika Kombe la Dunia la kwanza kuchezwa kwenye nchi ya Kiarabu, na ambayo tayari inakabiliwa na maudhi kadhaa, Morocco ilipata wafuasi wengi kwa hatua kubwa kama timu ya kwanza ya Kiarabu kufikia robo fainali na timu ya kwanza ya Kiafrika kufika nusu fainali.
Muda baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa, timu ya Ufaransa iliposhinda iliondoka uwanjani, wachezaji wa Morocco walibakia, wakijiburudisha na upendo uliofunika uwanja huo na rangi zao nyekundu na kijani.
“Tunafahari kabisa ya kweli juu ya timu hii… tayari tumeweka historia kwa hiyo hatuwezi kuwahukumu kwa mechi hii,” alisema Mohamad Alaoui, mwenye miaka 24, mwanafunzi wa Morocco ambaye alisema alikuwa amesafiri kutoka Uingereza kuja kuangalia Kombe la Dunia na alishuhudia michezo yote waliocheza timu ya Morocco.
“Nina furaha kuwa niliweza kufika hapa kushuhudia timu hii ikiwa uwanjani na nikapata fursa kuwaona wakipiga hatua hadi hapa walipofikia katika mashindano haya ya Kombe la Dunia, alisema Samira Idrissi, umri miaka 34.
Huko mjini Rabat, ambapo mashabiki walikusanyika katika migahawa kwa saa kadhaa kabla ya mchezo huo kuanza, mkusanyiko huo ulinyanyuka kuishangilia timu yao licha ya kufungwa.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters