Washabiki wa Argentina walikuwa wakiimba jina la Messi katika eneo la Souq Wakif baada ya mchezaji huyo maarufu kufunga bao lake la kwanza kwa njia ya penalti katika dakika ya 34 ya kipindi cha kwanza.
Bao la pili la Argentina lilifungwa na Julian Alvarez baada ya kukimbia na mpira kutoka kati kati ya uwanja na kutumia vyema makosa ya mabeki wa Croatia.
Katika mchezo huo ambao Argentina walionyesha mchezo mzuri wakiongozwa na Messi ambaye sasa ameshacheza kwa miaka 20 na sasa akiwa na umri wa miaka 35 ameonyesha kwamba yeye bado ni mwamba.
Washabiki waliendelea kumshangilia pia baada ya kutoa ya kutoa asisti nzuri katika dakika ya 69 ya kipindi cha pili na kuzalisha bao la tatu lililofungwa tena na Julian Alvarez.
Fifa waliandika katika mtandao wao wa tweeter "Mfungaji bora mpya wa muda wote wa Argentina kwenye Kombe la dunia" baada ya Messi kufunga bao lake kwa njia ya penalti.
Bada ya mechi hiyo washabiki wa Argentina waliendelea kuimba uwanjani na wachezaji wa timu hiyo walikuwa wakiruka ruka kwa furaha baada ya ushindi huu mkubwa katika historia ya timu yao.
Sasa Argentina wameingia fainali na watapambana na mshindi kati ya Ufaransa na Morocco ambaye atajulikana siku ya Jumatano.
Argentina wamerudia historia ya mwaka 1990 ambapo walifika fainali ya kombe la dunia licha ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Cameroon kwa bao 1-0.
Mwaka huu Argentina waliingia katika kombe la dunia na kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Saudia Arabia kwa bao 2-1.