Takriban Wamarekani 200 wa asili ya Kisomali kutoka kote Marekani walikusanyika nje ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani mwishoni mwa wiki kwa maandamano, wakitoa tahadhari kwa ghasia hizo.
Wanamgambo wa ndani wanapigana kuitenga mikoa mitatu - Sool, Sanaag na Cayn -- kutoka Somaliland ili kujiunga tena na Somalia. Wito wa mara kwa mara wa kusitisha mapigano hadi sasa umepuuzwa.
Baadhi ya waandamanaji wakiwa wamebeba bendera ya Somalia na mabango walionekana wakiimba kauli mbiu za kupinga vita, na kuunga mkono wahanga wa mapigano huko Las Anod, mji mkuu wa Sool.
Walitaka sitisho la mara moja, na bila masharti, kwa mapigano mjini Las Anod.
"Ni hatia kuwaua wasio na hatia, watoto, wazee, au wanawake. Somaliland haiwezi kutawala kwa nguvu. Hatutaruhusu Muse Bihi kuua watu wasio na hatia," alisema mmoja wa waandamanaji, Abdirashid Mohamed Farah.
Abdirahman Mohamed Abdi, waziri wa zamani wa uvuvi na rasilimali za baharini wa Somalia alikuwa miongoni mwa waandamanaji.
Rais wa Somaliland Muse Bihi alitangaza wiki iliyopita kwamba atatuma wazee wa koo kutafuta suluhisho la ghasia hizo.
Hata hivyo, wazee wa koo katika mji huo waliitaka Somaliland kuwaondoa wanajeshi wake kama sharti la mazungumzo.
Licha ya wito wa ndani wa kutaka amani na juhudi za kimataifa, ufyatuaji wa makombora na milio ya risasi iliendelea huko Las Anod Jumamosi, na kuua takriban watu 20, wakaazi na vyanzo vya hospitali viliiambia VOA.
Wasemaji wa pande zote mbili, waliozungumza na VOA walionekana kushutustumiana.
Msemaji wa wazee wa kimila huko Las Anod Garaad Abdikarim Ali alisema jeshi la Somaliland lilianzisha mashambulizi na kushambulia mji huo kwa mizinga Jumamosi.
Katika kujibu, msemaji wa Jeshi la Somaliland Abdi Dhere alisema wanamgambo wa eneo hilo, wakiungwa mkono na wanamgambo wa al-Shabab wameanzisha mashambulizi kwenye kambi ya jeshi la Somaliland.
Madaktari na hospitali za Las Anod walisema wiki hii kuwa watu 105 wameuawa na 602 wamejeruhiwa katika wiki tatu za mapigano.
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ilisema Jumatano mapigano huko Las Anod yamesababisha vifo vya watu 150 na wengine zaidi ya 600 kujeruhiwa tangu Februari 6.
Mwandishi wa VOA katika mji huo alisema mapigano yameongezeka wiki hii, huku pande zote mbili zikichimba mitaro kutetea misimamo yao, huku milio ya makombora na mizinga ikisikika kote.
Somaliland inachukulia eneo hilo kama sehemu ya eneo lake lililojitenga na inadai kwamba kujitoa kunaweza kuhatarisha juhudi zake za kutaka kutambuliwa kimataifa kama jimbo lililojitenga kutoka kwa Somalia.