Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 09:10

Vita vyazuka upya Gaza huku ripoti ikieleza Israel ilijua shambulizi la Oktoba 7


Wapalestina wakiwabeba watoto waliojeruhiwa kufuatia shambulizi la Israeli katika eneo la makazi, baada ya muda mfupi wa kusitishwa mapigano kati ya Hamas na Israel kumalizika huko Rafah, Kusini ya Ukanda wa Gaza.
Wapalestina wakiwabeba watoto waliojeruhiwa kufuatia shambulizi la Israeli katika eneo la makazi, baada ya muda mfupi wa kusitishwa mapigano kati ya Hamas na Israel kumalizika huko Rafah, Kusini ya Ukanda wa Gaza.

Mapigano kati ya Hamas na Israel yameanza tena huko Gaza baada ya siku saba za sitisho la mapigano lililowezesha kubadilishana mateka na wafungwa wa Palestina na kufikishwa misaada ya kibinadamu katika eneo lililoharibiwa na vita.

Majeshi ya Ulinzi ya Israel yalisema Ijumaa kuanza tena mapigano kunafuatia ukiukaji wa makubaliano ya muda mfupi na kikundi cha wanamgambo hao kurusha roketi kuishambulia Israel.

Ghasia hizo mpya zimekuja wakati gazeti la New York Times likiripoti kuwa Israel ilikuwa na taarifa ya kina kuhusu mpango wa Hamas wa kuishambulia Israel, lakini mpango huo ulipuuzwa kuwa ni “matamanio.”

Nyaraka hizo zilizotafsiriwa zenye kurasa takriban 40, zilizopewa jina “Jerico Wall” na kupitiwa na The Times, zilieleza jinsi Hamas watakavyo tekeleza mashambulizi mbalimbali katika ngome ya ulinzi ya Israeli na kuchukua miji kadhaa. Haikuweka kipindi cha tarehe ya shambulizi hilo.

The Times ilisema jeshi la Israeli na maafisa wa usalama walikuwa wanajua kuhusu mpango huo kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya shambulizi hilo la Oktoba 7. Haikuwa wazi iwapo Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alikuwa na taarifa.

Hapakuwa na maoni ya mara moja kutoka serikali ya Israeli kuhusu ripoti hiyo ya The Times.

Hata wakati milio na harufu za silaha kutokana na vita iliyorejea Gaza, wasuluhishi wa kimataifa wanaendelea na kutafuta njia ya kumaliza mapigano hayo.

Jeshi la Ulinzi la Israel lilisema kupitia mtandao wa kijamii wa X, uliokuwa zamani Twitter, kuwa “ulifanikiwa kuzuia” roketi hiyo iliyofyatuliwa kutoka Gaza.

Hakuna madai ya mara moja kutoka Hamas kuhusu kuhusika na shambulio hilo la roketi.

Wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas huko Gaza inasema takriban watu 32 wameuawa katika saa chache za awali Ijumaa wakati mapigano yalivyoanza tena.

Vipeperushi vilivyosambazwa na Israel huko Khan Younis kusini mwa Gaza vinawashauri watu huko kuondoka na kwenda eneo la mbali kusini kwa ajili ya usalama wao.

Wapalestina wakioka mikate katika eneo la kifusi cha nyumba zao zilizoharibiwa na mashambulizi ya Israeli wakati wa vita hivyo wakati wa sitisho la mapigano la muda kati ya Hamas and Israel, huko Khan Younis. REUTERS/Mohammed Salem
Wapalestina wakioka mikate katika eneo la kifusi cha nyumba zao zilizoharibiwa na mashambulizi ya Israeli wakati wa vita hivyo wakati wa sitisho la mapigano la muda kati ya Hamas and Israel, huko Khan Younis. REUTERS/Mohammed Salem

James Elder, msemaji wa UNICEF, alisema katika video iliyopachikwa katika mtandao wa X, kutoka hospitali “kubwa kabisa ambayo inaendelea kutoa huduma” kuwa “hospitali hii haiwezi kwa kifupi kuchukua watot zaidi wenye majeraha ya vita.” Amesema bomu limeanguka “kiasi cha mita 50 kutoka hapa.”

Elder alisema, “kutochukua hatua kwa wale wanaoweza kuzuia hili kumeruhusu mauaji ya watoto. Hii ni vita dhidi ya watoto.”

Kuanza tena mapigano kumekuja baada ya siku saba za kusitishwa mapigano zilizowezesha kubadilishana mateka wa Israeli waliochukuliwa na Hamas katika shambulizi la Oktoba 7 na wafungwa wa Palestina.

Baadhi ya taarifa katika habari hii inatokana na shirika la habari la AP, Agence-France-Presse na Reuters

Forum

XS
SM
MD
LG