Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 21, 2024 Local time: 16:09

Sitisho la mapigano la muda kati ya Israel na Hamas latekelezwa kwa siku ya sita


Mateka wa Israel walioachiliwa na Hamas wakiwa ndani ya helikopta ya kijeshi ya Israel, Novemba 24.
Mateka wa Israel walioachiliwa na Hamas wakiwa ndani ya helikopta ya kijeshi ya Israel, Novemba 24.

Sitisho la mapigano la muda kati ya Israel na Hamas limefikia siku ya sita leo Jumatano, huko pande zote mbili zikitarajia kuachiliwa kwa mateka zaidi na wafungwa wakati wapatanishi wanaendelea na juhudi za kutaka muda wa sitisho la mapigano uongezwe.

Msemaji wa usalama wa taifa wa Marekani John Kirby aliwaambia waandishi wa habari kwamba Marekani inashirikiana na Israel, Qatar na Misri ili sitisho la mapigano liendelee.

“Tunataka kuona mateka wote wakiachiliwa. Na njia ya kufanya hivyo ni kusitisha mapigano, Kirby alisema.

Makubaliano ya awali yaliitaka Israel kusitisha kwa siku nne mashambulizi yake yenye lengo la kuitokomeza Hamas, huku Hamas ikitakiwa kuwaachilia mateka 50, nayo Israel ikiombwa kuwaachilia Wapalestina 150 wanaofungwa jela.

Makubaliano hayo yaliruhusu pia upelekaji zaidi wa misaada ya kibinadamu Ukanda wa Gaza.

Sitisho la mapigano liliongezwa kwa siku mbili zaidi kwa masharti kuwa Hamas itawaachilia mateka 10 zaidi kwa siku, na Israel kuwaachilia wafungwa zaidi wa Palestina.

Jeshi la Israel limesema mateka 12 waliokuwa wanashikiliwa Gaza walifika Israel Jumanne usiku, na Israel iliwaachilia huru wafungwa wa Kipalestina 30, wanawake 15 na vijana wanaume 15.

Forum

XS
SM
MD
LG