Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 21:18

Majeruhi zaidi waokolewa kufuatia kuporomoka kwa jengo Kariakoo, Dar es Salaam


Ambulensi katika eneo ambapo jengo liliporomoka katika soko la Kariakoo, Dar es Salaam.
Ambulensi katika eneo ambapo jengo liliporomoka katika soko la Kariakoo, Dar es Salaam.

Ikiwa ni siku moja na saa kadhaa baada ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa nne katika soko la Kariakoo mjini Dar es Salaam, idadi ya waliofariki huenda imeongezeka kutoka watu watano na kufikia sita huku zaidi ya watu 70 wakiwa tayari wameokolewa.

Akizungumza na Sauti ya Amerika, Ileile Mavele, ambaye ni mfanyabiashara na mwokoaji katika eneo hilo amesema majeruhi wengine wawili wameokolewa huko mtu mwingine mmoja akidhaniwa kufariki Dunia.

‘’Muda huu watu wawili wametoka, kuna mtu mmoja ambaye kidogo afya yake si nzuri. Ila kuna mwingine alikuwa amening’inia mikono lakini amepelekwa hospitali ya Amana, hivyo anaendelea vizuri," Alisema Ileile.

Ileile ameishukru Serikali na wafanyabiashara kuungana kwa pamoja katika kipindi hiki, huku akiishauri serikali kuwa makini kuhusiana na vibali vya wahandisi.

Kwa upande wake katibu wa Wafanyabiashara katika soko la Kariakoo Riziki Ngaga, amesema jengo hilo lililoporomoka lilikuwa linatumiwa na watu zaidi ya 100, huku ikikadiriwa kulikuwa na idadi kubwa zaidi ya watu wakiwemo wafanyabiashara wakati linaporomoka mapema Jumamosi Novemba 16.

Wafanyakazi wa dharura vwakifanya kazi ya uwokozi kutoka jengo lililoanguka katika soko la Kariak, Dar es Salaam Novemba 16, 2024.
Wafanyakazi wa dharura vwakifanya kazi ya uwokozi kutoka jengo lililoanguka katika soko la Kariak, Dar es Salaam Novemba 16, 2024.

Hata hivyo Ngaga amesema kwa sasa wameishauri serikali kubadilisha ramani ya soko hilo kuendana na matumizi ya sasa hivi katika kujenga majengo haya.

‘’Sisi ni kuishauri Serikali, tumeishauri Serikali kwa kipindi hiki kutokana na kukua kwa Teknolojia, wasitumie zile sheria za zamani kwenye kujenga majengo haya. Kwa sababu kama majengo haya mengine yamejengwa miaka 20 iliyopita, matumizi ya miaka iliyopita ni tofauti na sasa.’’ Alisema Ngaga.

Asma Serungwi ambaye ni mfanyabiashara wa Kariakoo anasema kwa sasa hali ya biashara siyo nzuri kutokana na watu kuwa na huzuni na masikitiko makubwa kutokana na janga hilo, huku akiiomba serikali ijitahidi kuendelea kufanya uokoaji.

Awali Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila wakati akizungumza na waandishi wa habari, ameendelea kuwashukru kwa kuzidi kuwajuza Watanzania, na kuvishukuru vyombo vya ulinzi na usalama, raia na wafanyabiashara wa soko hilo huku akiwaomba watu wapuuze taarifa potofu zinazoenezwa na watu mitandaoni jkwamba uokoaji huo ulisitishwa jana usiku.

‘’Ndugu waandishi wa habari, jambo hilo halikuwa la kweli, kwa sababu hivi tunavyozungumza kuanzia katibu mkuu wa wizara, naibu waziri, manaibu makatibu wakuu tumekesha hapa.’’

Adha Chalamila amesema kwa sasa wataendelea na uokoaji huo hadi pale wataalamu watakaposema walibomoe jengo hilo au la, huku akiongezea kusema uokoaji unahitaji akili kubwa kuliko nguvu nyingi.

-Imetayarishwa na Egberth Alfred

Forum

XS
SM
MD
LG