Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 06, 2024 Local time: 02:41

UNICEF yasema watoto 90,000 hatarini DRC


Vita DRC yawanyima fursa ya watoto kwenda shuleni.
Vita DRC yawanyima fursa ya watoto kwenda shuleni.

Idara ya Umoja wa Mataifa ya kuhudumia watoto (UNICEF) inaripoti kuwa takriban watoto 90,000 wamelazimishwa kukimbia makawao kutokana na kusambaa kwa ghasia za kijamii huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) katika jimbo la Ituri.

Eneo la Djugu huko Ituri kaskazini mashariki mwa DRC limekuwa ni sehemu ya mauaji ya watu kukoseshwa makazi, huku maelfu ya watu wakikimbia nyumba zao kwa kukhofia maisha yao.

UNICEF imeripoti wiki iliopita kuwa ghasia za kikabila katika jimbo hilo zimewakosesha makazi kiasi cha watoto 66,000 ndani ya eneo na kusababisha wengine 25,000 kutafuta hifadhi katika nchi jirani ya Uganda.

Mizozo ya ghasia kati ya makundi ya kikabila ya wahema na walendu juu ya ng’ombe na maeneo ya malisho ilizuka mwezi Desemba, baada ya kuwepo na ukimya kwa kipindi cha takriban miongo miwili iliyopita. Mzozo kati ya makundi hayo mawili uliongezeka mapema mwezi huu kwa nguvu za uharibifu mkubwa.

Msemaji wa UNICEF, Christophe Boulierac, anasema kuwa zaidi ya vijiji 70 vimechomwa moto. Anasema zaidi ya watu 76 wamepigwa risasi na kufa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Boulieran anasema kuwa vituo vitatu vya afya na shule saba zimekumbwa na wizi au kuchomwa moto, na kuwanyima watoto fursa ya kupata elimu. Ameongezea kwamba elimu imevurugwa kwa kiasi cha watoto 30,000 katika zaidi ya shule 100 kote katika eneo hilo.

UNICEF imeonya kwamba maelfu ya watoto wako katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa wa kuharisha, kipindupindu na maradhi mengine kwasababu ya hali ya mbaya ya hewa, ukosefu wa chakula na maji safi. Idara hiyo inasema yeye na mashirika mengine ya misaada yanagawa mablanketi, sabuni, maji safi na misaada mingine muhimu kwa watu wenye shida.

UNICEF inatoa wito wa kupatikana kwa suluhisho la amani kwa mzozo, na kuelezea kuwa kumalizika kwa ghasia ndiyo njia pekee ya kuwalinda watoto kutokana na hatari nyingi wanazokabiliana nazo.

XS
SM
MD
LG