Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesema kuna uwezekano wa Russia kuwekewa vikwazo iwapo Kremlin haitatoa maelezo haraka juu ya kushukiwa kuhusika na kupewa sumu kwa kiongozi wa upinzani Alexey Navalny.
Heiko Maas ameliambia gazeti la Ujerumani Bild am Sonntag kuwa kulikuwa na “viashiria kadhaa” kuwa Moscow ilikuwa nyuma ya shambulizi hili la sumu.
“Kama katika siku zijazo Russia haitasaidia katika kufafanua kilichotokea, tutalazimika kujadili na washirika wetu namna ya kujibu hili,” Maas ameliambia gazeti la Ujerumani litolewalo kila siku, akiongeza kuwa vikwazo vyovyote vile “viwalenge.”
Hivi sasa Ujerumani ndio inaongoza Umoja wa Ulaya.
“Tuna matarajio makubwa ya serikali ya Russia kutatua uhalifu huu wa hali ya juu,” Maas amesema.
“Iwapo serikali haihusiki kwa namna yoyote na shambulio hili, hivyo ni kwa maslahi yake kuja na ukweli juu ya hili.”
Maas hakufuta uwezekano wa vikwazo dhidi ya mradi wa Nord Stream 2 wa bomba la Mafuta wenye thamani ya dola bilioni 11 ambalo linajengwa ili kufikisha gesi inayozalishwa na Russia kufika barani Ulaya.
“Ni matumaini yangu… kuwa Warusi hawatatulazimisha tubadilishe msimamo wetu juu ya Nord Stream,” amesema.
Ujerumani haitosita kuchukua hatua yeyote inayowezekana kusitisha mradi huo baada ya kufanya tathmini, Maas amesema, na kuwa mjadala juu ya vikwazo usiangaliwe kwa “ufinyu” kwa suala moja tu.