Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 19:32

Ujasiri, katiba ndio siri ya kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais Kenya


Dkt Kizza Besigye
Dkt Kizza Besigye

Wanasiasa Afrika Mashariki wamesema kuwa ili kufikia mabadiliko ya kweli ni lazima mahakama ziwe na ujasiri na wananchi wenyewe waidai katiba na kuisimamia.

Dkt Besigye

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Dkt Kizza Besigye amepongeza uamuzi wa Mahakama ya Juu nchin Kenya kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8 ambapo Rais Uhuru Kenyatta alichaguliwa tena kuongoza nchi hiyo.

Amesema kuwa majaji wa Kenya wameweza kuwa na ujasiri wa kufanya kile ambacho majaji wa Uganda wameshindwa kufanya hilo katika matukio ya kesi kama hiyo mara tatu.

Dkt Besigye alipinga matokeo katika Mahakama ya Juu mwaka 2001 na tena 2006 wakati kura zilipodaiwa kuibiwa ili kumpendelea Rais Museveni ashinde.

Katika matukio yote, mahakama ilikubaliana naye Dkt Besigye katika hoja nyingi, japokuwa hatimaye mahakama ikaamua kuwa dosari hizo hazikuweza kuathiri kwa kina matokeo ya uchaguzi huo.

Kwa hiyo amesema kuwa iwe basi inatosha kwa anayepinga matokeo kushinda iwapo ataweza kuthibitisha kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria.

Njelu Kasaka

Njelu Kasaka, waziri wa zamani enzi za utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, amesema ili kufikia mabadiliko ya Katiba ni lazima wananchi wenyewe waidai.

“Nawapongeza Wakenya kwa sababu wameweza kujitawala kwa kuweka uongozi wanaoutaka na kuuondoa wenyewe. Sisi tunaweza kufikia hatua hiyo kwa kudai Katiba nzuri na kuweka taasisi zitakazoisimamia, kama Bunge na Mahakama,” alisema Kasaka.

Alisema licha ya Tanzania kuwa mstari wa mbele katika vita ya ukombozi wa Afrika miaka ya sitini, imebaki nyuma kidemokrasia tofauti na nchi zilizokuwa nyuma.

“Tuliwalaumu makaburu wa Afrika Kusini kwa kukandamiza demokrasia, tukasema demokrasia itawale hadi Zimbabwe, lakini leo tumeshindwa kuwawajibisha viongozi wetu,” alisema.

“Wananchi waanze kudai Katiba mpya, lakini hatuwezi kuifikia kama hatuna kambi ya upinzani imara. (Kama) Bado hatujawa na vyama vya upinzani imara, kwa sababu kwa sasa vinabanwa na bado wananchi wengi hawaonyeshi mwamko. Lazima tusawazishe nguvu ili kupata mabadiliko.”

Pius Msekwa

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimeendelea kusema kuwa wakati ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta, ukiwa umebatilishwa na Mahakama ya Juu nchini Kenya, wanasiasa katika Afrika Mashariki wameendelea kusema kuwa wakati wa kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais mahakamani umewadia.

Wakati ibara ya 140 ya katiba ya Kenya inaruhusu mtu yeyote kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais mahakamani ndani ya siku saba tangu kutangazwa kwa mshindi, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bado inakataza.

Ibara ya 74(12) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema hakuna mahakama yoyote nchini itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba.

Hilo ni jambo ambalo limekuwa likijadiliwa tangu kubatilishwa kwa uchaguzi wa rais wa Kenya katika nchi za Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla. lakini Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Pius Msekwa alipoulizwa kuhusu hilo, Msekwa alisema muda umefika,“Jibu ni ndiyo.”

“Tunaweza kufikia hatua hiyo na tumeshaifikia. Katiba Mpya iliyopitishwa na Bunge mwaka 2014 inasema matokeo ya urais yanaweza kupingwa mahakamani. Katiba ya sasa hairuhusu, lakini katiba inayopendekezwa imeruhusu. Tunachosubiri ni referendum (kura ya maoni) tu,” aliongeza.

Msekwa amesema mchakato wa kubadili Katiba ulianzishwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka 2011 lakini ukakwama mwaka 2014 ukiwa katika hatua ya kura ya maoni baada ya NEC kueleza kuwa haikuwa na muda wa kutosha .

Hata hivyo, mchakato huo uliingiwa na dosari baada ya baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba, hasa kutoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD kuususia wakidai kuwa chombo hicho kiliacha Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuingiza ajenda za chama tawala.

Hata hivyo, wajumbe waliosalia waliendelea na mchakato na kupitisha Katiba Inayopendekezwa.

Hata hivyo, Rais John Magufuli ameshasema kuwa Katiba mpya si kipaumbele chake kwa kuwa kwa sasa anataka “kuinyoosha nchi”.

Kuhusu suala hilo, Msekwa alisema hawezi kuzungumzia utawala wa sasa kwa kuwa una utendaji wake.

“Mambo ya utawala wa sasa siwezi kuyasemea,” alisema Msekwa.

“Swali lako la msingi ni kama tunaweza kufikia hatua ya kupinga matokeo ya urais na nimesema ndiyo tunaweza.”

Kada Mkongwe wa CCM

Kada mkongwe wa CCM aliyewahi kuwa waziri katika utawala wa Mwalimu Julius Nyerere na ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini, alisema hata kabla ya kupata Katiba mpya vyama vya upinzani vilishakubaliana na Kikwete mambo manne, likiwemo la kupinga matokeo ya urais.

“Wagombea urais kupingwa mahakamani ni jambo zuri, “ alisema.

“Kimsingi vyama vya upinzani na na Rais Kikwete walishakubaliana baada ya mchakato wa Katiba kukwama. Sijui kwa nini hayakutekelezwa.

“Mambo manne waliyokubaliana ni kupinga matokeo ya urais, mgombea urais atangazwe kushinda akifikisha asilimia 50 na zaidi ya kura, kuwa na tume huru ya uchaguzi na kuwa na mgombea binafsi. walikubaliana kabisa, sijui kwa nini hayakutekelezwa. Waulize wapinzani.

Dkt Mohamed Bakari UDSM

Kwa upande wake Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt Mohamed Bakari alisema ili Tanzania ifikie mabadiliko ya Kenya, ni lazima mapambano ya kudai Katiba mpya yaongezeke.

“Ukichukua uzoefu wa Kenya, mpaka katiba imepatikana kulikuwa na mapambano makali sana yakihusisha vyama vya siasa, asasi za kiraia na wananchi wanaopenda demokrasia. Msukumo kama huo ni mdogo Tanzania,” alisema Dk Bakari.

XS
SM
MD
LG