Kikosi kazi kinachojumuisha mashirika mbalimbali kinaratibu juhudi za kukabiliana na mlipuko huo katika kambi mbili za wakimbizi katika eneo la Kyangwali na Kyaka.
Yona Tukundane ni afisa habari wa ngazi ya juu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa anasema:
"Hatua za kuzuia kuenea maradhi hayo zimechukuliwa ili kudhibiti ugonjwa huo na shughuli za ufuatiliaji zinaendelea ikiwemo kutembelea nyumba hadi nyumba, wagonjwa wenye rufaa, uchambuzi wa takwimu na vianzo vyake na hivi ninavyo zungumza timu za madaktari wanafanya kazi bega kwa bega na wizara ya afya."
Sio chini ya wakimbizi 26 wamekufa kutokana na mlipuko huo, na kuna zaidi ya wengine 600 wanashukiwa kuwa wamepatwa na kipindupindu.
Kipindupindu kinasababisha mtu kuharisha na kutapika na kupoteza maji mwilini. Ugonjwa huu unaweza kumuua mtu kwa muda wa masaa machache.
Ugonjwa huo huenezwa kupitia chakula na maji yaliyochanganyika na kinyesi cha mtu aliyepata maradhi hayo. Unaenea kwa haraka katika maeneo yasiyo na usafi na makazi yenye msongamano ambapo huduma za vyoo ni adimu hasa katika kambi zenye msongamano mkubwa wa wakimbizi
Katika kambi za wakimbizi ambazo zimeathiriwa na kipindupindu nchini Uganda, maafisa wa mashirika ya misaada wanasema huduma za maji na choo hazitoshelezi kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi wapya zaidi ya 40,000 ambao wamewasili.
Ahmed Mahat ambaye ni kiongozi wa Shirika la madaktari bila mipaka katika kituo cha matibabu kambi ya Kyangwalianasema:
Hivi sasa kiwango cha maji kwa kila mtu hakitoshelezi. Tunazo lita sita tu ambazo kila mtu anaweza kupatiwa anapofika sehemu ya mapokezi ya kituo hiki.