Wachambuzi wa kijeshi wamesema kuwa kitendo cha Marekani kuitungua ndege ya mshirika wa Russia huko Syria kumeamsha wasiwasi katika duru za wachambuzi wa kijeshi.
Wachambuzi hao wamekuwa wakihisi kuwa inawezekana kukatokea tukio la vita ya moja kwa moja kati ya Russia na Marekani, hata kama itakuwa kwa bahati mbaya, na kuweza kuingia katika mgogoro ambao hautaweza kuzuilika.
Ripoti zinaeleza kuwa ndege ya kivita ya Russia na ndege ya upelelezi ya Marekani Jumatatu zilikaribiana mita mbili, hali iliyoonekana kuwa “sio salama” kwa maoni ya jeshi la Marekani.
Ndege ya Russia aina ya SU-27 iliruka katika spidi ya juu karibu mno na ndege ya Markenai hali ilioonyesha rubani wake kutoweza kuimudu, amesema msemaji wa Pentagon.
Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema kuwa ndege aina ya RC-135 ya Marekani ya kijasusi ilifanya kitendo cha uchokozi kuikabili ndege ya kivita ya Russia.
Lakini makabiliano mengine ya karibu yalitokea baina ya pande mbili hizo Jumatano. Moscow imesema ndege ya kijeshi ya NATO ilipita kwa kasi karibu na ndege ya Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergei Shoigu wakati akielekea katika eneo la kijeshi la Russia huko Kaliningrad, lilioko kati ya wanachama wa NATO, Poland na Lithuania.
Vyombo vya habari vya Russia vimeripoti kuwa ndege ya kivita aina ya SU-27 ya Russia “iliifukuza” ndege ya kivita F-16 ya Polland na kuchapisha picha ya tukio hilo.
Kuna hatari wakati ndege moja inaporuka katika masafa ya karibu na ndege nyingine, kwa mujibu wa mchambuzi wa kijeshi Pavel Felgenhauer.
“Lakini huko katika eneo la Baltics, hiyo ndio hali halisi inayotayarisha hali ya hatari bila ya sababu… ikisababishwa na pande zote mbili,” amesema mchambuzi huyo.
Kwa hiyo ni kamchezo fulani ambao ni hatari. Lakini, ukweli ni kuwa, hakuna yoyote anayetaka kumshambulia mwenzie.
Kitendo cha ujasusi wa Russia dhidi ya wanachama wa NATO katika anga zao kimeendelea kuongezeka kwa haraka zaidi tangu Moscow ilipovamia kwa mabavu Rasi ya Crimean huko Ukraine na kuongezeka kwa msaada wa kijeshi kwa vikundi vilivyo jitenga vinavyosaidiwa na Russia katika mashariki mwa Ukraine.
Hakuna shaka, angalau kwa upande wangu, kuwa Russia na nchi za Magharibi ziko katika hali ya Vita Baridi mpya,” amesema mchambuzi huyo wa mambo ya Ulinzi Alexander Golts, Mhariri msaidizi wa Jarida la Yezhednevny Zhurnal la Moscow. Vita Baridi ni hali ambayo kunatatizo ambalo haliwezi kutatuliwa… sio kidiplomasia au kijeshi. Hili ndilo tatizo la Ukraine.