“Utafanyika mapema sana. Ninayo tarehe. Ninafahamu pahali utakapo fanyika,” alisema Trump. “Imeshakubalika na wote kufanyika.”
Kabla ya kuondoka Washington kwa ziara ya siku moja mjini Dallas, Jimbo la Texas, Rais aligusia kuwa sehemu na tarehe kwa ajili ya mkutano huo wa kihistoria vimeshathibitishwa na uongozi wa Korea Kaskazini.
Akiwa katika bustani ya Kusini mwa White House, rais huyo alisema kuwa serikali za Marekani na Korea Kaskazini zimekuwa zikiendelea kufanya mawasiliano na mazungumzo pia yamehusisha kuachiwa kwa Wamarekani watatu wanaoshikiliwa Pyongyang.
Wanaoshikiliwa ni Tony Kim na Kim Hak Song ambao walikuwa wakifundisha katika Chuo Kikuu cha Pyongyang cha sayansi na teknolojia, chuo pekee cha binafsi katika nchi hiyo. Wawili hao walikuwa wanashikiliwa kila mmoja kivyake mwaka 2017 na wanatuhumiwa kwa kushiriki na harakati za kuipinga serikali na kujaribu kuipindua serikali.
Mtu wa tatu anayeshikiliwa ni Kim Dong Chul, ambaye alikamatwa huko Rason upande wa kaskazini mashariki ya ncha ya Korea Kaskazini Octoba 2015. Alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela na kazi ngumu mwaka 2016 baada ya kukutwa na hatia ya ujasusi.