Msaada huu kupitia mpango wa dharura wa Rais wa nchi hiyo wa kukabiliana na ukimwi (PEPFAR) utaongeza idadi ya Watanzania wanaopatiwa matibabu ya kufubaza VVU kufikia milioni 1.2.
Aidha utaimarisha mapambano dhidi ya VVU kupitia huduma za upimaji, matibabu, kufubaza na kuzuia maambukizi ili hatimaye kufikia lengo la kutokomeza ukimwi ifikapo mwaka 2030.
Taarifa ya ubalozi wa Marekani nchini imesema fedha hizo zitafadhili miradi inayotekelezwa chini ya mpango wa utekelezaji wa PEPFAR utakaoanza kutekelezwa Oktoba hadi Septemba 2018, na ni ongezeko la asilimia 12.3 ya bajeti ya mwaka jana.
Bajeti iliyotengwa inajumuisha pia utoaji wa huduma na matibabu kwa watoto yatima na walio katika mazingira hatarishi pamoja na kukabiliana na ukatili wa kijinsia.
PEPFAR pia itasaidia mpango wa tohara ya hiari kwa wanaume, walengwa wakiwa 890,000.
Mpango huu unaendeleza ubia wa muda mrefu kati ya Marekani na Tanzania katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na muongo mmoja wa ushirikiano uliowezesha kudhibiti kwa mafanikio maambukizi ya VVU.
Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Virginia Blaser alisema, “Kwa pamoja tunafanya kazi ili hatimaye kuwa na kizazi kisicho na Ukimwi Tanzania – ambacho hakuna hata mtu mmoja anayeachwa nyuma.