Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Januari 24, 2025 Local time: 09:41

TLS yasema usalama wa wanasheria uko mashakani Tanzania


Rais wa TLS Tundu Lissu
Rais wa TLS Tundu Lissu

Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Godwin Ngwilimi, akifungua mkutano mkuu wa nusu mwaka Jumamosi,  amesema kuwa usalama wa wanasheria uko mashakani kuliko wakati mwingine wowote tangu kuanzishwa kwa chama hicho.

“Tunawalaani majahili na waovu hawa waliokusudia kuangamiza maisha ya rais wetu, tunahimiza vyombo vya dola kuharakisha uchunguzi wa tukio hilo. Sisi ni chombo ambacho kinahitajika na jamii, Serikali inatuhitaji na hata hawa wauaji wanatuhitaji.

“Kwa nini wajitokeze watu kutuangamiza? Lissu ameshambuliwa kwa risasi, ofisi za IMMMA zilivunjwa na jambo la kushangaza wezi hao hawakuchukua vitu vingine isipokuwa nyaraka, tena walilenga ghorofa ambayo ofisi hizo zipo, lakini wakiziacha ofisi zingine katika ghorofa za chini kwenye jengo hilo,” alisema Ngwilimi.

Vyanzo vya habari Jijini Arusha vimesema kuwa kabla ya kufunguliwa rasmi kwa mkutano huo, mawakili hao waliomba dua maalumu iliyoongozwa na Wakili Mchungaji Loita Lengai; kuwalaani wote walioshiriki katika tukio la kumshambulia kwa risasi Lissu.

Polisi yasema inafanya uchunguzi

Jeshi la Polisi nchini limeonyesha kutokuwa tayari uchunguzi wa tukio la Lissu kufanywa na vyombo vya mataifa ya nje, likisisitiza linaendelea kufanya uchunguzi.

Tamko hili limekuja siku moja tangu Mbowe kutoa wito wa Serikali kukubali vyombo vya nje ambavyo vinaaminiwa na pande zote (serikali na Upinzani) vifanye uchunguzi dhidi ya watu waliohusika kumshambulia kwa risasi, Lissu mchana kweupe ili ukweli upate kujulikana.

Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Barnabas Mwakalukwa amesema kwamba jeshi la polisi linafanya kazi kitaaluma.

“Sisi tunaendelea na uchunguzi, suala la mtu kuchukua watu wa nje ni yeye. Sisi tunaendelea kufanya uchunguzi, sisi ni ‘professional’ (wataalamu). Hatuwezi kumzuia mtu kuongea, kuna mtu mwingine anaweza kusema mimi siwezi kuendelea mahakamani au siwezi kuendelea na uchunguzi. Ana haki kikatiba kutoa maoni yake kusema lolote, yeye ni mwanasiasa, lakini sisi kama polisi tunaendelea na uchunguzi,” gazeti la Mtanzania limenukuu kamanda Mwakalukwa.

Chadema yataka uchunguzi kutoka nje

Katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi baada ya kurejea kutoka nchini Kenya alikokuwa kwa siku 15 kufuatilia kwa karibu matibabu ya Lissu, pamoja na mambo mengine, Mbowe alieleza shaka waliyonayo dhidi ya vyombo vya ulinzi na usalama vya hapa nchini katika kuchunguza suala hilo.

Alikwenda mbali akisema kuwa wanavishuku vyombo hivyo na hata kuwaona ni watuhumiwa namba moja katika tukio hilo kwa kile alichodai kuwa viashiria vyake vyote tangu linatokea, kauli za baadhi ya viongozi, kusita kwao, kujiosha na mazuio yasiyo na mantiki, vinaweza kumwelekeza mtu yeyote mwenye akili timamu kudai hayo.</p>

Ingawa Mbowe alisema hamjui ni nani ndani ya vyombo hivyo, lakini alidai kuwa si jambo la afya kwa watuhumiwa kujichunguza wenyewe.</p>

Alisema hata wao Chadema pamoja na kwamba kuna mkakati unatengenezwa wa kusema wamehusika kwa sababu ya kugombania vyeo, pia watakuwa tayari kuchunguzwa na hata kuchukuliwa na vyombo hivyo vya nje ili ukweli ujulikane.

Kamanda amtaka Mbowe awataje wahusika

Akijibu madai ya Mbowe ya kuvituhumu vyombo vya ulinzi na usalama kuwa ni watuhumiwa namba moja wa tukio hilo, Mwakalukwa alimtaka awataje wahusika au apeleke taarifa kwa siri ndani ya jeshi hilo.

“Kama ana-suspect, he can mention them, (anaweza kuwataja) because he knows them (kwa sababu anawajua), so its very easy to him even to (kwa hiyo ni rahisi sana kwake hata ku..) kuwatajia hata waandishi wa habari. If you have information deliver those information (kama una taarifa, toa),” alisema Mwakalukwa.

Mwakalukwa alisitiza kuwa kitendo cha kuendelea kulizungumza jambo hilo kunaweza kuharibu mwenendo wa uchunguzi.

Uchunguzi unafuata weledi

Kuhusu namna wanavyofanya kazi na kutumia mbinu za kisayansi, Mwakalukwa alisema: “Sisi polisi tunafanya kazi kisayansi, tunazingatia weledi, tunafanya kazi kwa kuzingatia usasa, usasa inamaanisha nini, tuna tovuti yetu, tuna nini, we are professional.“Tumepeleleza kesi nyingi kwa kushirikiana na mataifa mbalimbali, leo hii unasema kwamba unataka kufanyaje, ni mawazo yake na hatuwezi kuzuia mawazo ya mtu,” alisema Mwakalukwa.

Juzi Mbowe alisema wamezungumza na vyombo vya uchunguzi kutoka nchi za Marekani, Uingereza, Ujerumani na vyote viko tayari kuja kutoa msaada.

Alisema vyombo hivyo vinachohitaji sasa ni maombi kutoka Serikali ya Tanzania.

“Kama mnajiamini hawa watu waje kufanya uchunguzi, msibaki tu mnasema ni Chadema wenyewe kwa wenyewe, ruhusuni watu wenye utaalamu wao waweke vielelezo hapa,” alikaririwa Mbowe.

Kauli ya Jaji Mkuu

Alisema hapingani na kauli ya Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kuwa vyombo vya ndani havijashindwa kufanya uchunguzi, lakini mtuhumiwa namba moja ni vyombo vya ulinzi na usalama.

Mbowe alisema hadi wao kudai vyombo huru vya uchunguzi kunatokana na madhila ya muda mrefu ambayo vyombo vya ndani vya ulinzi na usalama vimeonyesha havina msaada katika hilo.

Mbowe asisitiza washambuliaji wanajulikana

Katika hilo, Mbowe alikumbushia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, ambaye alidai waliomshambulia wanajulikana na hakuna aliyefikishwa mahakamani.

Zaidi alikumbushia kupotea kwa msaidizi wake, Ben Saanane na kwamba alimuuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuhusu Serikali kuruhusu uchunguzi huru kutoka Scotland Yard, lakini alikataa.

Kauli hiyo ya sasa ya Jeshi la Polisi inafanana na ile iliyotolewa kabla ya hapo na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Juma na Mkuu wa Majeshi nchini, Venance Mabeyo.

XS
SM
MD
LG