Mkutano wa mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani alioufanya na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki umekuja miezi miwili baada ya kuripotiwa kuwa Trump alitumia maneno machafu kuelezea nchi ya Haiti na baadhi ya nchi za Afrika.
Umoja wa Afrika na serikali kadhaa za Afrika walikuwa wamekasirishwa na matamko hayo ya Trump.
“Nafikiri ahadi ya mafungamano ya Marekani na nchi za Afrika iko wazi juu ya umuhimu tunaotoa katika ushirikiano huu. Rais ameandika barua yake binafsi kwenda AU,” amesema Tillerson katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Faki huko makao makuu ya AU mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Faki amesema alipokea barua iliyoandikwa Januari 25 na “tukio hili” tayari ni “jambo lililopita.”
Faki ameongeza kuwa ziara ya mwanadiplomasia wa juu wa Marekani ni ushahidi kuwa mahusiano kati ya Afrika na Marekani bado ni imara.”
Tillerson amesema kuwa kuhamasisha amani na usalama, maendeleo na biashara, na utawala bora ni nguzo tatu zinazotumiwa na Washington katika kushirikiana na Afrika.