Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 18:58

Tanzania yailaumu Canada baada ya mkulima wa Afrika Kusini kukamata ndege yake


Palamagamba Kabudi, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Tanzania
Palamagamba Kabudi, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Tanzania

Ndege ya Tanzania aina ya Bombardier Q400 imekamatwa nchini Canada.

Taarifa iliyotolea na Wizara ya Mambo ya Nje imesema kuwa Waziri Palamagamba Kabudi amethibitisha kukamatwa kwa ndege hiyo. Kwa mara nyingine ndege ya nchi hiyo imekamatwa nchini Canada.

Waziri ameeleza masikitiko yake ya kukamatwa kwa ndege ya Tanzania nchini Canada siku chache kabla ndege hiyo mpya kuondoka nchini humo kuja Tanzania.

Ndege mpya ya Tanzania aina ya Bombardier Dash 8 - Q400 iliyokuwa ikitengenezwa nchini Canada imekamatwa kwa amri ya Mahakama nchini humo kufuatia mkulima mstaafu raia wa Namibia Hermanus Steyn kufungua kesi ya madai dhidi ya Tanzania.

Steyn, anaidai serikali ya Tanzania fidia ya dola milioni 33 baada ya mali zake kutaifishwa nchini humo mwaka 1980.

“Tayari Steyn alishashindwa mara tatu katika Mahakama ya Tanzania na Afrika Kusini baada ya Mahakama nchini humo kuamuru kushikiliwa kwa ndege ya Tanzania aina Boeing 787 – 8 Dreamliner Agosti 2019,” amesema Waziri Kabudi.

Akizungumza katika hafla ya kuapishwa kwa Mabalozi watano wa Tanzania iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma, Kabudi ameelezea kusikitishwa na kitendo cha ndege za Tanzania kukamatwa mara tatu katika kiwanda cha Bombardier nchini Canada wakati ndege aina ya Boeing 787 – 8 Dreamliner zinazotengenezwa nchini Marekani hazikamatwi zinapotoka nchini humo kuja Tanzania.

Waziri amesema tayari amemuita Dodoma, Balozi wa Canada hapa nchini ili kueleza kwa nini Canada inaruhusu vitendo hivyo vya kibeberu kufanyika nchini kwake.

Amefafanua kuwa Tanzania inatambua kuwa katika kipindi hiki ambacho imeamua kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha uchumi wake wapo mabeberu wanaofanya jitihada za kukwamisha juhudi hizo, wakiwatumia vibaraka wa ndani na nje ya Nchi na kwamba haitaruhusu vitendo hivyo vikwamishe jitihada za Tanzania kujiimarisha kiuchumi.

“Kwa mara ya tatu ndege ambayo ilikuwa ifike Tanzania, imekamatwa Canada na kesi ipo Mahakamani, na aliyefanya hivyo ni mtu yuleyule ambaye alikamata ndege yetu Afrika Kusini, tukaenda Mahakamani tukamshinda, akakata rufaa na wiki iliyopita akashindwa tena nchini Afrika Kusini, huyohuyo amekimbilia Canada amekamata ndege aina ya Bombardier Q400 ambayo ilikuwa ifike nchini na jambo linalosikitisha ndege aina ya Dreamliner mbili kutoka Marekani hazikushikwa na zimefika.

Kila ndege zinapotaka kutoka Canada tunashangaa hao watu, hao matapeli wanajuaje na ndege zinakwenda kukamtwa, jana nilichukua hatua ya kumuita Balozi wa Canada hapa nchini na alifika Dodoma, nimemwambia kinaga ubaga, bila kupepesa macho, bila tashwishwi kwamba hatufurahishwi kabisa na tabia na vitendo hivi vya kila ndege yetu inapotakiwa kuondoka Canada kurudi Tanzania inakamatwa, na nimemwambia sio tu hatufurahishwi bali tumekasirika.

Kabudi aliongeza kuwa : “Hivyo tunafikiri Mhe. Rais kukushauri, kama Canada inaendelea kufanya vitendo kama hivyo sio wao pekee yao wanaotengeneza ndege, hatukufanya makossa kwenda kununua ndege Canada zipo nchi nyingine, hata Brazil wanatengeneza ndege”

Haiwezekani kila ndege inapotakiwa kwenda kufanya majaribio inasikingiziwa leo hali ya hewa mbaya halafu baadaye inakamatwa, lazima kuna mchezo mchafu,ndege hizi hununui kwa faida yako, wala faida ya familia yako, na unisamehe, Mhe. Rais nimeona leo bora niseme ili Watanzania waelewe kwamba unafanya juhudi kubwa lakini wapo wanaokesha usiku mzima wananguruma ili wairarue nchi hii kama simba”amesema Mhe. Prof. Kabudi.

Waziri Kabudi amesema pamoja na hatua ya kumuita Balozi wa Canada, Serikali imechukua hatua nyingine za kusimamia jambo hili ikiwa ni pamoja na kupata wanasheria na tayari hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa.

Ndege mpya aina ya Bombardier Dash 8 Q400 ambayo ingekuwa ndege ya 8 kuwasili hapa nchini kati ya ndege 11 zilizonunuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano ilipangwa kuwasili hapa nchini tarehe 28 Novemba, 2019.

Kabudi amewataka Mabalozi walioapishwa kupigania maslahi ya Tanzania katika nchi wanazowakilisha huku wakitambua kuwa wapo mabeberu wasioitakia mema Tanzania na wanakesha wakifanya juhudi za kukwamisha kila jitihada zinazofanywa kuijenga Tanzania.

XS
SM
MD
LG