Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Novemba 24, 2024 Local time: 02:03

Tanzania: Kupanda kwa bei za nafaka kwaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wa kawaida


Soko la Kariakoo, mjini Dar es Salaam, Tanzania
Soko la Kariakoo, mjini Dar es Salaam, Tanzania

Kupanda kwa bei za nafaka katika masoko nchini Tanzania  kumeongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wa kawaida kutokana  na umuhimu wa bidhaa hizo kugusa maisha ya kila siku.

Wakati huo huo wataalamu wa uchumi wameishauri serikali kubuni mikakati ya muda mfupi na mrefu ili kuweza kudhibiti bei.

Hali ya bei za nafaka imezidi kuwa gumzo kwa wananchi wengi huku wale wenye vipato vya kawaida wakiendelea kupata maumivu kutokana na bidhaa hizo kupanda maradufu kila mara jambo linalofanya ugumu wa maisha kuongezeka huku vipato vikiwa havitoshelezi

Mhadhiri Msaidizi wa kitivo cha usimamizi wa biashara chuo kikuu huria cha Tanzania Vicent Stanslaus akizungumza na Sauti ya Amerika amesema Serikali inahitaji kuwekeza kwa kuwa na kilimo cha umwagiliaji ambacho hakitategemea mvua pamoja na kujenga viwanda vya mbolea nchini ili kuwasaidia wakulima kurahisisha kilimo na kupunguza gharama.

“Kwa hiyo tukifika kwenye hatua yakuwa na kilimo cha umwagiliaji ambacho hakitegemei mvua moja kwa moja kilimo kinakuwa kimestaimilika na bei zinaenda kushuka lakini nikipindi cha muda mrefu sio muda mfupi. Pia hata kujenga viwanda vya mbolea vinavyo tengenezwa hapa nchini vinasaidia pia kwenye kupunguza mfumuko wa bei kwenye eneo la vyakula kwa kipindi cha muda mrefu, ” aliongezea Stanslaus.

Aidha wataalamu hao wanasema kupanda kwa bei za nafaka kila siku ikwemo mahindi, mchele na ngano kumechangia kwa kiwango kikubwa kuwaumiza wananchi kufuatia gharama za maisha kuongezeka hivyo kuitaka Serikali kutatua jambo hilo kwa mikakati ya muda mrefu na mfupi pia.

Mmoja wa wataalamu hao Dkt Eliaza Mkuna ambaye ni msimamizi katika idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, amesema Serikali inatakiwa kufuatilia kwa karibu udhibiti wa gharama za pembejeo pamoja na kuwataka wakulima kuwa waaminifu katika upangaji wa bei zao.

“Bei imepungua kutoka laki moja na arubaini kuja mpaka elfu sabini lakini bado gharama zinakuwa kubwa ya viwatilifu pia wakulima wenyewe masoko haya tunayo yazungumzia na msimu ambao unakuja sasa tunategemea kwamba uwaminifu uwepo katika upangaji wa bei na serikali isiweze kuingilia moja kwa moja ” amesema Dkt Eliaza

Kwa upande wake Profesa. Aurelia Kamuzora ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la uwezeshaji wananchi Kiuchumi nchini Tanzania amesema tatizo kubwa lililochangia kupanda kwa bei ni uhuru wa kuyaachia masoko yapange bei bila ya kuingiliwa na Serikali hali ambayo imekuwa ni maumivu kwa wanunuzi na wakati huo wakulima wakiwa hawapatiwi ruzuku katika ununuzi wa mbolea na hivyo kulazimika kupandisha bei za mazao yao.

“Kwahiyo ukipeleka mbolea watu watazalisha zaidi inavyoenda kuongeza uzalishaji wa mahindi na watu wakapata mahindi yakutosha mahindi yatakapo kuwa mengi kwenye soko basi hizo bei za nafaka zitashuka,” alisema Kamuzora

Hata hivyo Profesa Kamuzora amesema Kama Serikali itashindwa kutoa ruzuku kwa wakulima ongezeko la bei linaloshuhudiwa ksasa huenda likaongeza maradufu hali itakayowatesa zaidi wananchi walio wengi.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhan, Tanzania.

XS
SM
MD
LG