“Vipimo vya maabara vilivyofanyika katika maabara ya huko Kagera na baadaye kuthibitishwa jijini Dar Es Salaam, vilibaini mgonjwa mmoja alikuwa na virusi vya Marburg,” alisema katika mkutano na baadhi ya maafisa wa serikali na wizara ya afya ambao ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus mjini Dodoma.
Wiki iliyopita, waziri wa afya alikanusha kuwepo kwa mlipuko huo katika taifa hilo la Afrika Mashariki akisema hakuna mtu yeyote aliyeambukizwa virusi hivyo.
Ilikuwa baada ya WHO kusema kwamba ilipokea ripoti za kuaminika kwamba watu wanane walifariki kutokana na virusi vinavyoshukiwa kuwa Marburg katika eneo hilo hilo tarehe 10 Januari.
Waathirika walikuwa na dalili kama za Marburg, ikiwemo maumivu ya kichwa, homa kali, maumivu ya mgongo, kuhara, kutapika damu, udhaifu wa misuli na kutokwa na damu.
Virusi hivyo vya homa kali ya kutokwa na damu vinasababisha kifo kwa asilimia 88, ni sawa na virusi vya Ebola, na vinaambukizwa kwa binadamu kutoka kwa popo kwenye maeneo ya Afrika Mashariki.
Rais Samia alisema serikali imeimarisha juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo na kwamba timu ya kukabiliana kwa haraka na virusi hivyo ilipelekwa huko Kagera kufuatilia kesi zote zinazoshukiwa na kujaribu kudhibiti mlipuko huo.
Alisema, watu wote 25 walioshukiwa kuwa na Marburg hawakuambukizwa virusi hivyo.
Tedros alisema WHO itatoa dola milioni 3 kwenye mfuko wake wa magonjwa ya dharura kusaidia katika juhudi za kudhibiti mlipuko huo nchini Tanzania.
Forum