“…Namuonya ameshatupa taarifa atuache tufanye kazi kwa mujibu wa sheria. Na akiendelea tutamchukulia hatua za kisheria bila kuathiri taarifa alizotuletea,” alisisitiza.
Alitoa onyo hilo pia kwa watu wengine, wanaofikiri kuwa wanaweza kuishinikiza Takukuru na kuiingiza katika masuala ya kisiasa kuwa wakome, kwani inafanya kazi wa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo.
“Hiki ni chombo kinachojiendesha kwa mujibu wa sheria, hakishinikizwi wala kuingiliwa na mtu yeyote. Na kinapokea kwa mujibu wa sheria na taratibu taarifa za siri au wazi kutoka kwa mtu yeyote, Nassari anachokiita ushahidi sisi tunakiita taarifa mpaka pale uchunguzi wetu utakapokamilika,” alisisitiza Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Kamishna Valentino Mlowola.
Vyanzo vya habari nchini humo vimesema kuwa Kamishna alisema mbunge huyo kwa takribani mara tatu alifika katika ofisi za Takukuru na kuwasilisha kile alichokiita ushahidi, lakini mara baada ya kuwasilisha taarifa hizo kwa Takukuru huitisha mkutano wa waandishi wa habari na kuelezea yale yaliyojadiliwa na taasisi hiyo.
Alisema Oktoba 2, mwaka huu, mbunge Nassari akiambatana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, wote wa Chadema, walifika katika ofisi za Takukuru na kuwasilisha taarifa zao kuhusu matukio ya rushwa yaliyotokea mkoani Arusha.
Alisema Oktoba 14 pamoja na Oktoba 16, mwaka huu, Nassari pia aliwasilisha tena maelezo yake kuhusu suala hilo la rushwa kwa Takukuru na kila alipoondoka alifanya mkutano na waandishi wa habari na kuelezea yaliyojiri wakati akiwasilisha taarifa hizo.
Mkuu wa Takukuru alisema kwa mshtuko taasisi hiyo ilishangaa kuona mbunge huyo na wenzake, wakifanya vikao na waandishi wa habari na kuzungumzia kwa undani yaliyojiri hadi yale ambayo hayakupaswa kuzungumzwa kutokana na kuharibu uchunguzi.
Alisema kazi ya Takukuru ni kupokea taarifa za rushwa na ubadhirifu na kuzifanyia uchunguzi wa kina na ikisha thibitika kuwepo kwa tatizo, hufungua jalada na kuliwasilisha katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa ajili ya hatua za kisheria kuchukuliwa.