Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 21:31

Sitisho la matangazo lazuiliwa na Mahakama Kenya


Raila Odinga akiapishwa
Raila Odinga akiapishwa

Jaji wa Mahakama Kuu jijini Nairobi Chacha Mwita ametoa agizo la kusitisha mara moja marufuku iliotolewa na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kwa vyombo vya habari.

Hatua ya vyombo vya habari husika kukiuka agizo la serikali ya Rais Kenyatta kutopeperusha matangazo mubashara kwenye uapisho wa kiongozi wa upinzani (Nasa) Raila Odinga kutoka bustani ya Uhuru Jumanne ndiyo sababu kuu iliyoikasirisha serikali ya Kenya.

Kupitia halmashauri ya mawasiliano serikali imeamrisha kuzima runinga ya mashirika ya habari ya Citizen na Inooro zinazomilikiwa na Royal Media Services, NTV inayomilikiwa na Nation Media Services na KTN na KTN News zinazomilikiwa na Standard Media Group.

Serikali imeendelea kusisitiza kuwa runinga hizo nne zitaendelea kuzimwa hadi serikali ikamilishe uchunguzi kubaini uhusiano wa vyombo hivyo vya habari na upinzani.

Jaji Chacha Mwita ameagiza marufuku hiyo ya serikali kusitishwa mara moja na kuziruhusu runinga hizo kupeperusha matangazo.

Jaji amesisitiza kuwa amri hiyo ya mahakama itadumu hadi wakati ambapo kesi iliyowasilishwa na mwanaharakati Okiya Omtatah itasikilizwa na kuamuliwa Februari 14.

Mpaka wakati tukichapisha habari hii runinga hizo tatu zilikuwa bado zimezimwa, lakini Okiya Omtatah ambaye aliwasilisha kesi mahakamani anaeleza Idhaa ya Sauti ya Amerika kuwa iwapo serikali itakaidi agizo hilo la mahakama atawasilisha kesi mpya kuishtaki serikali ya Rais Kenyatta.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa serikali pia imeagizwa na mahakama kutohujumu utendakazi wa vyombo vya habari nchini Kenya.

Hata hivyo baraza la vyombo vya habari nchini Kenya limeitaka serikali kufutilia mbali marufuku ya kuzizima runinga hizo,wanaharakati wa haki za kibinadamu vile vile wameishtumu serikali.

Mkurugenzi wa Amnesty International nchini Kenya, Houghton Irungu: "Ni lazima iwe wazi kuwa kitendo kilichotekelezwa na serikali kuzima runinga hizi kubwa za kibinafsi sio tu ni jambo geni kwa katiba ya Kenya bali pia ni tisho kwa demokrasia yetu, na ni lazima ipingwe na kuwa runinga hizo zirudishwe hewani mara moja.

Nick Hailey, Balozi wa Uingereza nchini Kenya amepaza sauti yake na kuitaka serikali kuviruhusu vyombo vya habari kufanya kazi yake kwa njia huru.

Ameendelea kusema:" Ningependa kuihimiza serikali jinsi nimesema awali kuviruhusu vyombo vya habari kufanya kazi yake kwa njia huru si kwamba ni jambo zuri kufanya lakini ni kwa sababu inachangia kuimarisha na kuboresha sura ya Kenya ulimwenguni."

Mpaka hivi sasa serikali haijatoa taarifa yoyote kuhusu kadhia hii ya mahakama, lakini kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa mara ya kwanza baada ya kula kiapo Jumanne, kando na kusisitiza kuwa vinara wanne wa muungano huo wako pamoja, anaeleza kuwa uhuru wa vyombo vya habari sharti uheshimiwe.

Raila Odinga ameuliza: "Nani amempa Bw Matiang’I nguvu hizo anazojigamba kuwa nazo? Tufuate katiba ya Kenya ama tusiifuate na tutengane."

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Nairobi.

XS
SM
MD
LG