Chilima alikuwa ndani ya ndege ya kijeshi na watu wengine tisa ilipoondoka mjini Lilongwe nyakati za asubuhi, ofisi ya Rais wa Malawi ilisema katika taarifa ya awali.
Ilisema juhudi za mamlaka ya usafiri wa anga kuwasiliana na ndege hiyo tangu ilipopotea kwenye mitambo ya rada hazikufaulu. Ndege hiyo ilitarajiwa kutua kwenye uwanja wa ndege wa Mzuzu saa nne asubuhi majira ya huko.
Ndege hiyo haikuweza kutua kwenye uwanja huo kutokana na hali mbaya ya hewa na kuamriwa kurejea katika mji mkuu, Rais Lazarius Chakwera alisema katika hotuba yake kwa taifa kwa njia ya televisheni.
“Ninayo matumaini kwamba tutawapata manusura,” alisema, akiongeza kuwa shughuli za kuitafuta ndege hiyo zimejikita karibu na eneo la kilomita 10 katika hifadhi ya msitu.
“Nimetoa maagizo kamili kwamba shughuli hiyo iendelee hadi ndege ipatikane,” alisema.
Alisema Malawi iliwasiliana na nchi jirani, na serikali za Marekani, Uingereza, Norway na Israel kusaidia katika juhudi za ukoaji.
Forum