Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 15:29

Upinzani washinikiza 'Scotland Yard' ichunguze kupotea kwa Ben Saanane


Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani nchini Tanzania Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani nchini Tanzania Freeman Mbowe

Upinzani Bungeni Tanzania umeendelea kuishinikiza serikali kutoa maelezo juu ya kutekwa na kupotea kwa watu akiwemo Ben Saanane, suala ambalo limesababisha hali ya hofu kubwa kwa wananchi.

Kiongozi wa kambi ya upinzania Freeman Mbowe amesema hivi sasa imetimia miezi sita tangu msaidizi wake Ben Saanane kupotea katika hali ya kutatanisha na serikali haijatoa tamko lolote kuhusu suala hilo, akiomba serikali kuwasiliana na shirika la upelelezi la Scotland Yard la Uingereza kusaidia katika upelelezi.

“Tunafahamu kuwa Scotland Yard wanaweledi mkubwa katika kuchunguza matatizo kama haya na waliwasaidia Kenya wakati walipokuwa katika matatizo kufanya uchunguzi juu ya mauaji ya siri ya Dkt Robert Ouko, wakati huo akiwa kiongozi mashuhuri katika nchi hiyo," amesema.

“Kwa nini serikali isingewasiliana na shirika la upelelezi la Uingereza ambalo linautaalamu wa hali ya juu katika kutafuta vielelezo vya uchunguzi, ilikusaidia uchunguzi wa kupotea kwa Ben Saanane,” amesema Mbowe.

Akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amethibisha kuwa Tanzania inauhusiano mzuri na mataifa mengine, na kuwa tunashirikiana nao katika masuala ya upelelezi.

Lakini amesisitiza kuwa vyombo vya upelelezi nchini Tanzania pia vinauwezo mkubwa katika kufanya uchunguzi juu ya masuala yanayolikabili taifa, vyanzo vya habari mjini Dodoma vimeeleza.

“Hatuwezi kukurupuka kutoa tamko kwa umma kwa hivi sasa… uchunguzi bado unaendelea… na tunaweza kupoteza vyanzo vya taarifa za upelelezi ambao wanaweza kusaidia na vielelezo vinavyoeleza kwanini mambo haya yanatokea. Ninapenda kusisitiza kuwa wananchi waendelee kutupatia ushirikiano… katika kutupa fununu juu ya suala hili,” Waziri Mkuu ameeleza.

“Serikali haijaemewa kwa hali yoyote ile… au katika uchunguzi wa aina yoyote na wakati uchunguzi juu ya matukio yaliotokea nchini ukikamilika, repoti hiyo itawekwa wazi kwa umma. Bado tunawasihi Watanzania kufanya subira na kuwa na imani na serikali yao na vyombo vyake vya usalama,” alisema Waziri Mkuu.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani alitaka ufafanuzi juu ya kusitishwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.

Waziri Mkuu amesema kuwa Watanzania bado wanaendelea kupokea repoti za mambo yanayoendelea katika Bunge wa utaratibu uliokubalika.

Akizungumzia suala la wabunge kutaka kuwepo matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, Mwanasheria Mkuu George Masaju aliwataka wabunge kutambua kuwa, kinachotakiwa ni kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha ili waendelee kukubalika kwa wananchi wao.

Wakati huo huo Mwanasheria Mkuu amesema serikali haijakataza vyombo vya habari kutoa taarifa kwa umma, bali imefanya mabadiliko kwenye taratibu za kutoa habari hizo.

Katika kujibu shutuma hizo kutoka kambi ya upinzani amesema kuwa kama mnavyojua vyombo vya habari kama magazeti havijazuiliwa kuripoti mambo yanaendelea bungeni.

“Kama `Bunge Live’ lingekuwa suluhisho la kutambulika kwa kazi za wabunge, basi asilimia zaidi ya 70 ya wabunge walioanguka katika uchaguzi wa mwaka 2015 wasingepata anguko hilo la kisiasa, kwa kuwa matangazo yalikuwa yanarushwa moja kwa moja. Naomba kushauri kuwa tusitumie vibaya uhuru wa mijadala,” amesema.

Na hata huku kutangazwa inaitwa matangazo mubashara, someni ibara ya 100 kama ipo hiyo haki someni sheria ya haki, kinga na madaraka ya bunge kama iko hiyo haki, amesema Mwanasheria Mkuu huyo.

“Someni kanuni 143 haki tuliyonayo ni taarifa za bunge ibara ya 18 ya katiba inatoa haki ya watu kupewa taarifa. Niwashauri waheshimiwa wabunge kama mtataka kurudi kwenye bunge hili, teteeni mambo yanayowahusu wapiga kura wenu, matangazo mubashara hayawasaidii chochote,” alisema Masaju.

Hali kadhalika alitumia fursa hiyo kuwaomba wenye taarifa kuhusu kupotea kwa aliyekuwa Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ben Saanane washirikiane na jeshi la Polisi ili kufanikisha kupatikana kwake.

“Wenye taarifa wakiwemo waliokuwa wakifanya naye kazi watoe ushirikiano kwa polisi ili kuweza kupata ufumbuzi wa hili na kujua alipo Saanane,” alisema.

Mbali na hilo, aliwataka wabunge kutotumia vibaya uhuru unaotokana na nyadhifa zao. Alisema ingawa wabunge wanapewa uhuru wa kuzungumza wanapokuwa bungeni, bado wanapaswa kuchunga mipaka na haki za wengine katika kuwasilisha na kushughulikia mambo mbalimbali yaliyo kwenye majukumu yao.

XS
SM
MD
LG